• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 11:55 AM
Umma unateseka sababu ya ufisadi – Wetang’ula

Umma unateseka sababu ya ufisadi – Wetang’ula

Na GAITANO PESSA

SENETA wa Bungoma Moses Wetang’ula amewakashifu baadhi ya magavana kuhusu ufisadi katika kaunti zao, akisema wamesababisha wakazi kuhangaika kutokana na ukosefu wa huduma muhimu.

Alisema wakazi hawanufaiki kutokana na fedha zinazosambazwa kwenye kaunti na serikali kuu kutokana na usimamizi mbaya kimaksudi kutoka kwa baadhi ya maafisa wa kaunti huku magavana wakitazama tu.

“Raslimali za kaunti ni za wakazi na wala si za watu wachache waliojawa na ubinafsi. Pindi tutakapofaulu kuwezesha fedha zaidi kusambazwa mashinani ni muhimu kwamba kila mtu atafurahia matunda ya ugatuzi,” alisema.

Bw Wetang’ula ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Ford Kenya alisema Seneti itapigia debe uwajibikaji kuhusu raslimali za kaunti na haitachoka kushinikiza kukamatwa kwa magavana fisadi wanaofikiri hawawezi kuathiriwa na sheria za nchi.

“Kila baada ya miaka mitano huwa tunachagua watu kama magavana lakini mwishoni mwa hatamu yao tunakumbana na uhalisia wa kuzalisha mabilionea. Tunaunga mkono kikamilifu serikali kuu katika vita dhidi ya ufisadi katika viwango vyote vya kitaifa na vya kaunti ili kulinda fedha za umma,” alisema seneta huyo. Aliwataka wanaoshinikiza ulinzi wa magavana ambao wamehusishwa na ufisadi kufikiria tena uamuzi wao wasije wakaonekana kama maadui wa uwajibikaji na makuhani wa utapeli.

“Hakuna yeyote katika taifa hili aliye juu ya sheria. Hata Rais amelindwa tu na Katiba akiwa angali afisini lakini baada ya hatamu yake atawajibikia vitendo vyake.

“Kwa sababu hii, wote walioshtakiwa kuhusiana na ufisadi ni sharti wabebe msalaba wao hadi watapothibitishwa vinginevyo na taasisi husika,” alisema Bw Wetangula.

You can share this post!

Mhudumu wa mochari alilia korti aendelee kuvuta bangi

Wazee walalamika kutolipwa pesa za uzeeni mwaka mzima

adminleo