UN-Habitat yalia kuhusu ukosefu wa fedha na raslimali za kutosha
Na MAGDALENE WANJA
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa kuhusu Makazi (UN-Habitat) limewaomba wafadhili pamoja na mataifa ambayo ni wanachama kutoa fedha za kuwezesha kutekeleza miradi.
Akizungumza wakati wa mkutano na bodi ya usimamizi, Mkurugenzi Mtendaji Maimunah Mohd Sharif alisema kuwa shirika hilo linahitaji fedha ili kutekeleza miradi ila kwa sasa hazipo.
“Nayaomba mataifa ambayo ni wanachama na wafadhili kutusaidia ili tuweze kutekeleza majukumu yetu,” akasema Bi Sharif.
Bi Sharif aliyechukua usukani katika ngazi ya uongozi UN-Habitat Januari 2018 alisema kuwa alipata shirika hilo likiwa tayari linapitia changamoto kifedha na kiraslimali.
“Ilibidi tuchukue hatua kama vile kusimamisha shughuli za kuwaajiri watu upya na kufikia sasa kuna nafasi za kazi 34 ambazo hajijajazwa,” akasema Bi Sharif.
Aliyapongeza mataifa kama vile Kenya na Norway kwa kuongezea mchango wao kila mwaka.
Kufikia sasa, Kenya imeongeza mchango wake kutoka Sh70 milioni hadi Sh100 milioni.
Kulingana na Waziri wa Uchukuzi, Miundombinu, Nyumba na Maendeleo ya Mijini, James Macharia, Kenya imejikakamua katika kuunga mkono kazi na wajibu wa UN-Habitat.
“Ninatoa changamoto kwa mataifa ambayo ni wanachama kutimiza ahadi zao na yale ambayo hayajatoa ahadi yoyote yajitolee ili kuunga mkono kazi za shirika la UN-Habitat,” alisema Bw Macharia.
Baadhi ya miradi ya UN-Habitat nchini ni pamoja na ujenzi wa nyumba chini ya mradi wa makazi kwa gharama nafuu yaani “affordable housing”.