UNDP kutumia teknolojia kuboresha mazingira ya safari za ndege Afrika
Na FAUSTINE NGILA
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa kuhusu Mipango ya Maendeleo (UNDP) linapigia upatu matumizi ya teknolojia kusaidia bara la Afrika kurejelea safari za ndege na biashara katika mazingira salama katika kipindi ambapo dunia inajiandaa kuwapa chanjo mabilioni ya watu dhidi ya virusi vya corona.
Shirika hilo limeshirikiana na Umoja wa Afrika kupitia AfroChampions katika utekelezaji wa mradi wa utambulisho wa kidijitali kwa jina PanaBIOS, utakaotumiwa katika viwanja vya ndege na mipaka ya mataifa yote barani.
Mradi huo unawezesha abiria wa ndege kupimwa na matokeo yake kutumika kushauri kuhusu mazingira salama ya kufanyia biashara yasiyo ya maradhi hayo.
Bw Achim Steiner, ambaye ni afisa msimamizi wa UNDP aliambia Taifa Leo kuwa mojawapo ya mbinu madhubuti za kuzuia kuyumba kwa uchumi wa dunia ni kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa kuimarisha maendeleo.
“Mradi huuu wa PanaBIOS ni mfano bora kwa makuu tunayoweza kufikia iwapo tunaweka juhudi na fikra zetu pamoja,” alisema.
Kupitia ushirikiano huo, mtandao huo wa data ya kiafya utatumia teknolojia za blockchain na zile za kiotomatiki kuunda vyeti maalum vya kidijitali vya matokeo ya kupimwa na chanjo kwa muda mfupi kwenye viwanja vya ndege. UNDP ilisema mradi huo unawiana na ule wa Global Haven.
“Global Haven ni mradi wa kidijitali wa kuleta maendeleo kwa watu wote. Bara la Afrika limetoa mfano mwema kwa mabara mengine kufuata kwa kuzindua mradi huu,” alisema Ahunna Eziakonwa, mkurugenzi wa Afrika katika UNDP.
Kuhakikisha kuwa matumizi ya teknolojia yamedumisha haki za kibinadamu hasa katika matumizi ya data ya kiafya, UNDP imesema itawekeza kwa mpango wa udhibiti, uhamasishaji na uwazi.