UNESCO yazidi kumtambua Grace Ogot kwa mchango wake katika jamii
Na Victor Rabala
MAREHEMU Dkt Grace Ogot anaendelea kusifiwa miaka minne baada ya kifo chake, kwa mchango wake wa kupigania masuala aliyoamini yangesaidia kuboresha maisha ya wananchi.
Dkt Abdul Rahman Lamin kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), alitaja kuwa Bi Ogot anaendelea kutambuliwa kwa kutetea haki za wanawake na elimu kwa wote, kujitolea katika huduma za umma, upendo kwa familia na jamii.
“Tunajua sasa yuko salama mikononi mwa mababu zetu na jukumu letu ni kuendeleza na kutunza sifa bora alizoacha,” akasema Dkt Lamin, aliyezungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa UNESCO Afrika Mashariki, Bi Ann Theresa Ndong Jatta, eneo la Gem Yala, Kaunti ya Siaya.
Mumewe, Prof Bethwel Ogot alimsifu marehemu kama mtu aliyejitolea kuhakikisha jamii nzima inanufaika. Walizindua pia kitabu chake cha nne kilichochapishwa baada yake kufariki, pamoja na sanamu ya Bethwel na Grace Ogot ambayo imewekwa katika lango la boma lao.
Bi Ogot alikuwa mwandishi maarufu wa fasihi. Aliandika vitabu vya riwaya kwa lugha ya Kiingereza amabvyo vilisifiwa kote nchini. Vitabu hivi ni The Promised Land, Land Without Thunder, The Strange Bride, The Graduate, The Other Woman, The Island of Tears. Vitabu vya The Royal Bead (2018) na Princess Nyilaak vilichapishwa 2018.
Alifariki mnamo Machi 18, 2015.