Upasuaji wa mwili wa Kenei wakosa kufanyika
NA MARY WAMBUI
UCHUNGUZI wa maiti ya marehemu sajini Kipyegon Kenei aliyekuwa akihudumu katika afisi ya Naibu Rais, Jumatatu ulikosa kufanyika kama ilivyopangwa.
Mpasuaji mkuu wa maiti Dkt Johansen Oduor, aliyefaa kufanya upasuaji huo ili kutegua kitendawili cha kiini kifo cha Bw Kenei, alieleza Taifa Leo kwamba alikuwa jijini Mombasa kikazi.
“Niko Mombasa kwa sasa. Nilifaa kufanya uchunguzi huo lakini huenda ukafanyika Jumatano,” akasema Dkt Oduor.
Matokeo ya uchunguzi huo yanatarajiwa kupiga jeki jitihada za wachunguzi kubaini kilichosababisha kifo cha afisa huyo.
Ripoti za mwanzo za polisi zilionyesha kwamba Bw Kenei alijitoa uhai, lakini ushahidi zaidi kutoka wachunguzi unatilia shaka ripoti hiyo.
Baada ya kifo cha afisa huyo, wachunguzi wa DCI walipiga kambi nyumbani kwake Nairobi wakikusanya ushahidi ambao unaashiria mwendazake hakujiua jinsi ilivyodaiwa.
Kinachotilia shaka madai kwamba afisa huyo alijinyonga ni jeraha la risasi lililokuwa kwenye kichwa chake.
Tayari wachunguzi wamethibitisha kwamba kijikaratasi kilichopatikana karibu na mwili wake hakikuandikwa na mwendazake.
Ijumaa iliyopita, familia ya afisa huyo iliomba polisi wahakikishe kwamba uchunguzi wa kina unaendeshwa ili wafahamu kilichosababisha mauti ya mwanao.
Kifo cha afisa huyo kimezingirwa na utata ikizingatiwa kilitokea wakati uchunguzi unaendelea kuhusu sakata ya utapeli wa ununuzi wa vifaa vya kijeshi Sakata hiyo imehusishwa na aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa na watu wengine watatu.