• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
USAJILI KDF: Wanawake wafungiwa nje

USAJILI KDF: Wanawake wafungiwa nje

NA KALUME KAZUNGU

WANAWAKE waliojitokeza kwenye Bustani ya Kibaki mjini Lamu wakati wa shughuli ya kusajili makurutu kuingia jeshini Jumatatu walilazimika kurudi nyumbani mapema baada ya afisa msimamizi kutangaza kutokuwa na nafasi zozote zilizotengewa jinsia ya kike eneo hilo mwaka huu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa shughuli hiyo, Afisa Msimamizi wa eneo la Lamu Magharibi, Luteni Kanali, Paul Aruasa, alisema kaunti ya Lamu iko na wanawake wengi ambao tayari wanahudumia jeshi la Kenya (KDF), hatua ambayo alidai ilichangia wanawake wa Lamu kufungiwa nje wakati wa shughuli ua usajili wa makurutu mwaka huu.

Bw Aruasa aliwataka wanawake waliojitokeza kutokufa moyo kwani huenda wakajumuishwa kwenye shughuli ijayo ya usajili wa makurutu nchini.

“Raundi hii hatuchukui wanawake. Kuna wanawake wa kutosha kutoka Lamu wanaohudumia kwenye kikosi cha jeshi la Kenya. Hii ndiyo sababu kuu iliyochangia Lamu kutopatiwa nafasi kwa akina dada mwaka huu. Wasubiri. Huenda raundi nyingine wakapewa nafasi,” akasema Bw Aruasa.

Baadhi ya akina dada waliojitokeza kwa shughuli hiyo aidha walieleza kutoridhishwa kwao na hatua ya kufungiwa nje ya zoezi hilo.

“Hii ni mara yabngu ya tatu kujaribu nipate nafasi ya kujiunga na KDF bila mafanikio. Nitaendelea kujaribu siku sijazo. Ombi langu kwa serikali ni kwamba watuzingatia sisi akina dada. Tunaweza,” akasema Bi Loice Kazungu.

Shughuli ya usajili wa makurutu kuingia jeshini ikiendelea eneo la Kibaki Grounds mjini Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

Naye Bi Emmaculate Muthee alitaja hatua ya kufungiwa nje ya zoezi hilo kuwa isiyofaa.

Alisema kubna haja ya kitengo cha jeshi kuwa na usawa wa kijinsia badala ya kuwapa kipaumbele wanaume pekee.

Bi Susan Wangoi ambaye yuko na miaka 35 alisema ndoto yake ya kujiunga na KDF imefifia kwani tayari amepitisha umri licha ya kujaribu mara kadhaa kila shughuli ya kusajili makurutu kuingia jeshini inapoandaliwa eneo hilo.

Wakati huo huo, visa vya makurutu kutemwa kutokana na meno yaliyobadilika rangi kutokana na utafunaji wa miraa pia vilikithiri wakati wa zioezi hilo.

Kadhalika makurutu waliokuwa wamejichora vibonzo kwenye miili yao na wale ambao walikuwa na uzani hafifu pia walitemwa nje ya zoezi hilo mapema.

Zaidi ya makurutu 200 walijitokeza kwenye shughuli hiyo.

You can share this post!

JAMVI: Ni mlima kwa Ruto kumnasa Mudavadi

#AFCON2019: Mataifa 14 yafuzu

adminleo