Thamini wateja wako, mkuu wa Username ashauri baada ya tuzo
NA FAUSTINE NGILA
KAMPUNI za Kenya zimetakiwa kuwathamini wafanyakazi na wateja wake katika utendakzi wake ili kuboresha mazingira ya kazi.
Afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Username Investment Limited, Bw Reuben Kimani alisema hayo baada ya kutawazwa mshindi wa Tuzo ya 2019 Realtor Founder of the Year katika dhifa iliyoandaliwa majuzi ya Tuzo za Waasisi wa Mwaka hapo The Nairobi Cinema.
Akiwashukuru wafanyakazi wake kwa hatua kampuni hiyo imepiga katika miaka iliyopita, Bw Kimani alizitaka kampuni kutambua haja ya kuwadhamini wateja wake ili kujiongezea mapato.
“Imekuwa safari ya kujitolea na kutokata tamaa. Nimejifunza mengi katika mazingira ya biashara, hakuna njia ya mkato ya kufaulu. Naamini kuwa Mola ametujalia nguvu za kipekee na vipaji ainati.
“Nawahimiza wakuu wa kampuni kuwadhamini wanunuzi wa bidhaa zake pamoja na wafanyakazi wanaojitolea kwa kila mbinu. Nawarai wajasiriamali ibuka kufanya utafiti wao kwanza ili kung’amua mapeno yaliyomo sokoni kisha kuwekeza kwa nafasi wanazopata, hapa Kenya na Afrika,” akasema Bw Kimani huku akipokezwa tuzo na Bw Ian Mbugua.
Dhifa hiyo iliwakutanisha waasisi katika vitengo mbalimbali, kama vile ardhi, kilimo bishara, fasheni, teknohama na elimu.
Hayo yalikuwa makala ya nne ya tuzo hizo zinazoandaliwa kila mwaka kuwatambua na kuwapa zawadi waasisi vijana ambao wanachangia pakubwa kujenga uchumi wa nchi.
Bw Kimani aliwataka Wakenya kuwekeza hela zao mahali zinaweza kukua kwa kasi, akitaja uwekezaji katika ardhi kama mojawapo ya maamuzi ya busara kwani unaweza kupata faida ya asilimia 25.8 ikilinganishwa na sekta zingine ambazo mapato hukua kwa asilimia 12.3.
Kabla ya tuzo hii, Bw Kimani pia alishinda tuzo ya 2019 African Business Personality Award aliyokabidhiwa na Voice Achievers Awards kutokana na biddi yake katika kuwezesha vijana kumudu bei ya uwekezaji wa ardhi barani Afrika.