Habari Mseto

'Ushauri wa Uhuru kwa vijana wa kiume wanaotafuta wapenzi'

October 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amewashauri vijana wa kiume wanaomezea mate mabinti katika jamii.

Rais ambaye ni mzazi wa watoto watatu wanaojumuisha wana wa kiume wawili na binti mmoja, alisisitiza kuhusu hitaji la wanaume kuheshimu wanawake hata wakati wanapojaribu bahati yao ‘kutupa chambo’.

“Nyinyi vijana (wa kiume) kama mnataka mwanamke, hamstahili kwenda kumkosea heshima. Wewe nenda (utupe chambo) polepole. Ukibahatika sawa, ukikosa tafuta mwingine,” akasema Rais Kenyatta.

Awakejeli madiwani waliompiga vita Elachi

Kiongozi wa nchi alionekana kutoa kauli hiyo ya wanaume kutongoza wanawake kwa mzaha akirejelea vurugu zilizotokea katika Bunge la Kaunti ya Nairobi wakati Spike Beatrice Elachi aliporejea afisini.

Ghasia hizo zilisababishwa na madiwani wanaume wakiongozwa na kiongozi wa wengi Abdi Guyo waliopiga kurejea kwa Bi Elachi ambaye aliungwa mkono na madiwani wanawake na wale wa chama cha ODM.

“Wazee waheshimu akina mama. Sio kuenda na kukosea mwanamke heshima,” Rais Kenyatta akasema huku wananchi wakiangua kicheko.

Wiki jana bunge la Kaunti ya Nairobi liligeuzwa uwanja wa vita madiwani kadhaa wanaume walipopinga kurejea kwa Bi Elachi.

Ilibidi polisi kurusha vitoa machozi ndani ya ukumbi huo kuwatawanya madiwani hao.

Mali ya thamani kubwa iliharibiwa, simu za mkononi zikaibiwa na wahuni walioingia ndani ya ukumbi wa mjadala kuungana na pande kinzani katika vita hivyo.

Alikuwa akizungumza katika hafla ya kuanzisha ujenzi wa barabara kuu ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA, hadi eneo la Westlands, Nairobi.

Akiwa ameandamana na Gavana wa Nairobi Mike Sonko pamoja na viongozi wengine, Rais alitoa wito kwa wananchi hasa vijana wasikubali kufuata wanasiasa kikondoo na kuchochewa kuanzisha vita dhidi ya wenzao kwa misingi ya kisiasa.

Amani na utulivu

Alitetea ushirikiano wake na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, na kusema ulikusudia kuleta amani ambayo imechangia utulivu unaowezesha shughuli za serikali kuendelea bila kutatizwa.

“Tulishindana na Raila lakini hiyo haimaanishi yeye ni adui yangu. Kushindana ni sawa lakini kuishi ni pamoja,” akasema.

Baadaye aliongoza pia shughuli ya kuanzisha ujenzi wa Kituo cha Makasha ya Shehena mjini Naivasha.

Kwa sasa ujenzi wa awamu ya pili ya SGR imepitia vituo vya Ongata Rongai, Ngong, Mai Mahiu na Suswa, ikihofiwa ufadhili haujapatikana kuendeleza ujenzi huo hadi Naivasha inavyokusudiwa.

Lakini Rais Kenyatta alihakikishia wananchi fedha zitapatikana kukamilisha mradi huo ilivyokusudiwa.