Habari MsetoSiasa

Ushirikiano wa Kalonzo na Uhuru hauwasaidii Wakamba – Prof Kibwana

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA PIUS MAUNDU

MWENYEKITI wa chama cha Wiper Prof Kivutha Kibwana kwa mara nyingine amejitokeza kumshtumu vikali kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka hii ikiwa dhihirisho tosha ya tofauti kubwa kati ya viongozi hao wawili wa chama hicho kinachoshabikiwa mno maeneo ya Ukambani.

Prof Kibwana amesema kwamba makubaliano ya kisiasa kati ya Bw Musyoka na Rais Uhuru Kenyatta hayana manufaa yoyote kwa jamii za Wakamba kwasababu yaliafikiwa visivyo na hayajumuishi ajenda ya kuleta maendeleo kwa jamii hiyo.

“Rais anazingatia sana kutimiza nguzo nne za maendeleo katika utawala wake. Tunafaa kujua kwa kiasi ganu sisi viongozi wa jamii ya Wakamba tunaweza kuyafikia maendeleo kwa watu wetu. Hata juzi tulipozuru ikulu hatukujitayarisha vyema kuwasilisha ajenda yetu ya maendeleo jinsi anavyofanya kinara wa NASA kwa sasa,” akasema Bw Kibwana kupitia taarifa iliyoonekana na Taifa Leo.

Matamshi ya gavana huyo yanaajiri baada ya Bw Musyoka kupitia hotuba yake Ijumaa iliyopita wakati wa kusheherekea tamaduni ya jamii ya Wakamba kudai kwamba aliamua kushirikiana na Rais Kenyatta kuimarisha vita dhidi ya ufisadi na kuhimiza umoja na amani nchini.

“Stephen Kalonzo Musyoka amekuwa ofisini tangu mwaka wa 1985, Charity Ngilu tangu 1992, Kivutha Kibwana tangu mwaka wa 2002 na Dkt Alfred Mutua mwaka wa 2013. Naona kwamba ni wakati wa jamii yetu kutuita akiwemo seneta wa zamani wa Machakos Johnstone Muthama ili tuwaeleze kile tumewatekelezea miaka hiyo yote na azimio letu la baadaye,” akasema Prof Kibwana kupitia taarifa hiyo.

Moja ya changamoto anazokumbana nazo Bw Musyoka ni wito wa Prof Kibwana unaomtaka atumia ushirikiano wake na Rais Kenyatta kutupa chambo kwa mahasimu wake wa kisiasa kama gavana Dkt Mutua na baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka jamii hiyo waliyoungana na chama cha Jubilee na kupoteza kura kwenye uchaguzi 2017.

Hii kulingana na gavana huyo wa Makueni itamsaidia Bw Musyoka kuweka msingi thabiti kwenye ngome yake ya kisiasa kisha kumweka pazuri katika jitihada za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa vigogo wa kisiasa wa jamii nyingine.

Kutokana na namna viongozi wanaomuunga Bw Musyoka mkono wamekuwa wakijipiga kifua na kushtumu wakosaoji wake, Prof Kibwana haamini kwamba makamu huyo wa rais wa zamani anatilia maanani ajenda ya maendeleo ya jamii ya Wakamba.

Wabunge Gideon Mulyungi, Daniel Maanzo, Rose Museo na seneta wa Kitui Enoch Wambua na baadhi ya madiwani wateule wamekuwa wakimkashifu Prof Kibwana, Bi Ngilu na Bw Mutua kama wanaotumiwa na maadui wa Bw Musyoka kuigawanya jamii ya Wakamba ili kusambaratisha azma yake ya urais mwaka wa 2022.