USHURU: Kiwango cha hela zinazopitishwa kwa simu chapungua
Na BERNARDINE MUTANU
Kiwango cha pesa zilizopitishwa kwa simu kimepungua huku serikali ikiendelea kutekeleza ushuru mpya kwa pesa zinazotumwa au kupokelewa kwa njia ya simu au benki.
Kulingana na takwimu kutoka kwa Shirika la Kitaifa la Kukusanya Takwimu (KNBS), kiwango hicho kimepungua sana kwa kuzingatia thamani ya pesa zilizopitishwa na nambari ya watu waliotuma au kupokea pesa kwa njia ya simu.
Kulingana na KNBS, kiwango cha pesa zilizopitishwa kwa njia ya simu kilipungua kwa zaidi ya Sh20 bilioni kutoka Sh348 bilioni Agosti hadi Sh327 bilioni mwezi wa Septemba.
Upungufu huo ni mkubwa sana ikizingatiwa kuwa katika kipindi kama hicho 2017 kiwango cha pesa zilizopitishwa kwa simu kilikua kwa Sh14 bilioni na Sh16 bilioni kati ya Julai na Agosti 2018.
Majuma kadhaa yaliyopita, serikali ilianza kutekeleza ushuru mpya kwa lengo la kukuza mapato yake kutoka kwa sekta ya simu za mkononi.
Katika Mswada wa Fedha 2018, Rais Uhuru Kenyatta alipendekeza ushuru maradufu kwa ada za kuweka au kutoa pesa benki na kwa kutumia simu kutoka asilimia 10 hadi asilimia 20.
Huduma za simu ziliongezewa ushuru wa thamani ya bidhaa (VAT) wa asilimia 15 na ushuru wa bidhaa (excise) kwa huduma za simu na matumizi ya intaneti.