Utata kuhusu umiliki wa shamba la ekari 134 waendelea kortini
Na RICHARD MUNGUTI
MRITHI wa mali ya bwanyenye Horatius Dagama Rose aliambia Mahakama Kuu Jumanne kwamba hajui mwaka baba yake marehemu alipouziwa shamba la ekari 134.4 liloko mtaani Karen, Nairobi na benki ya Barclays.
Bw Dimitri Da Gama Rose aliyekuwa anatoa ushahidi mbele ya Jaji Elijah Obaga aliungama kwamba hajui siku kampuni ya Muchanga Investments Limited (MIL) ambayo wakurugenzi wake ni makamu wa rais wa zamani Moody Awori na baba yake marehemu ilipouziwa shamba hilo.
Hata hivyo alisema hati ya umiliki wa shamba hilo ilitolewa na Wizara ya Ardhi mwaka wa 1983. Akihojiwa na mawakili wanaomwakilisha mjane Camerlina Mburu, Dimitri hangeweza kusema mwaka kamili shamba hilo lilipouzwa kati ya 1978 na 1982.
Barua nyingi ziliandikwa na kampuni za mawakili ya Kaplan & Stratton na Francis Da Gama Rose, babuye Dimitri kuhusu malipo ya kununua shamba hilo.
“Kutokana na wingi wa mabarua haya siwezi kusema Benki ya Barclays iliafikiana lini na Muchanga kuhusu kuuzwa kwa shamba hili lenye thamani ya Sh8bilioni lililoko mtaa wa kifahari wa Karen,”alikiri Dimitri.
Umiliki wa shamba hilo unang’ang’aniwa na mjane Carmelina Mburu, MIL,aliyekuwa meneja msimamizi wa hazina ya malipo ya uzeeni Josephert Konzollo kupitia kwa kampuni yake ya Telesource.Com Limited.
Bi Mburu aliyemteua Bi Catherine Njeri kuwasilisha kesi hiyo ameeleza mahakama shamba hilo ni la mumewe, marehemu John Mburu, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Nairobi miaka ya 1970’s.
Bi Mburu amesema mumewe alikuwa amepewa shamba hilo na serikali na kwamba alipoaga hati miliki ya shamba hilo liliibwa na shamba likauzwa.
Bw Konzollo anasema aliuziwa shamba hilo kwa bei ya Sh96milioni na Bw John Kamau. MIL inasema lilinunua shamba hilo kutoka kwa benki ya Barclays mwaka wa 1982 kwa bei ya Sh 1,250,000.
Benki ya Barclays ilikuwa imeteuliwa na mmiliki wa shamba hilo tangu 1919 Bw Arnold Bradley.
Akihojiwa na mawakili William Arusei, Pauline Kiteng’e na Kenneth Kamau, Dimitri alisema kumekuwa na barua chungu nzima kuhusu suala la uuazaji wa shamba hilo kati ya 1978 na 1983.
Benki ya Barclays ilikuwa imesimamia shamba hilo lililokuwa linamilikiwa na mlowezi Arnold Brondley. Hati ya umiliki wa shamba hilo zaonyesha kuwa Bw Brondley alipewa shamba hilo 1919.
Maerehemu Mburu alipewa umiliki wa shamba hilo 1977 kwa kipindi cha miaka 999.
“Je ni mwaka upi baba yako marehemu alinunua shamba hilo. Nyaraka mbali mbali zaonyesha Horatius alikuwa ameelezewa kuhusu ununuzi wa shamba hilo Januari 1 1979,” Bw Kamau alimwuliza Dimitri.
Akijibu Dimitri alisema , “ Ushahidi nilio nao waonyesha kuwa hatimiliki ya shamba hili lilikabidhiwa MIL mnamo 1983. Huo ndio wakati naweza sema shamba ilitwaliwa na MIL.”
Mahakama ilifahamishwa kuwa tarehe kamili ya kuuzwa kwa shamba hilo halijulikani.
Akiendelea kutoa ushahidi Dimitri alisema babuye Francis Da Gama Rose aliandikiwa barua na wakili Kaplan & Stratton akimweleza akamilishe kulipa Sh1.250,000 kwa benki ya BBK kisha shamba liandikishwe kwa jina la MIL.
Alieleza korti kuwa baba yake marehemu Horatius alikuwa ameajiriwa na babuye katika kampuni yake ya mawakili ya Francis Da Gama Rose kisha akajiuzulu akaanza kazi ya biashara.
Mahakama ilifahamishwa kampuni ya MIL haijawahi nunua shamba lingine ila hilo la Karen. Lakini awali benki ya Barclays ilitoa ushahidi ikisema haikuuza shamba hilo la Karen na kuzua kizugumkuti aliyeuzia MIL shamba hilo.
Mbali na Bi Mburu na MIL pia aliyekuwa meneja msimamizi wa hazina ya malipo ya uzeeni Josphert Konzolllo kupitia kwa kampuni yake Telesource alisema aliuziwa shamba hilo na Bw John Kamau kwa bei ya Sh96 milioni.
Kupitia kwa wakili Cecil Miller MIL ilifaulu kusimamisha shamba hilo likigawanywa na kuamuru lililindwe na maafisa wa polisi.
Afisa mkuu wa polisi eneo la Lang’ata aliagizwa na Mahakama kuu ahakikishe hakuna mtu ameingilia umiliki wa shamba hilo. Jaji Obaga atendelea kusikiza kesi hiyo kesho (Novemba 11, 2020).