Utata madiwani watatu sasa wakikanusha kupiga kura kubandua Nyaribo
KUTIMULIWA kwa Gavana wa Nyamira, Amos Nyaribo, kumechukua mwelekeo mpya baada ya madiwani watatu wa Bunge la Kaunti ya Nyamira kukana kuwa walishiriki upigaji kura wa kumwondoa madarakani.
Madiwani Julius Nyangana, Elijah Abere na Priscilla Nyatichi waliandikisha taarifa ya malalamishi katika Kituo cha Polisi cha Nyali, Mombasa ambako walikuwa wakati wa upigaji kura.
Ilisemekana watatu hao waliwaidhinisha madiwani wenzao wapige kura ya kumng’oa Bw Nyaribo kwa niaba yao.
Sasa wanadai hawakuidhinisha yeyote awapigie kura. Pia wamemshutumu Spika Thaddeus Nyaboro kwa kupotosha umma kuwa walitoa haki yao ya upigaji kura kwa wengine.
“Sikumtuma yeyote apige kura kwa niaba yangu wakati wa hoja ya kumtimua gavana. Nimeshindwa cha kufanya lakini niliandikisha taarifa Mombasa na kuwaambia mawakili wangu wachukue hatua,” akasema Bi Nyatichi.
“Nitaenda kortini kudumisha hadhi yangu kwa sababu nilikuwa Mombasa wakati ilidaiwa nilipiga kura. Nikiona saini na muhuri basi nitajua nani alisema apige kura kwa niaba yangu,” akaongeza.
Diwani huyo pia alisema anataka kufahamu ushahidi kutoka Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kuthibitisha iwapo aliongea na mtu ampigie kura.
Bw Abere naye alikanusha vikali kuwa aliamrisha apigiwe kura akisema hakuzungumza na mtu yeyote kuhusu suala hilo.
Mnamo Jumanne wiki jana, Bw Nyaribo aliondolewa madarakani ambapo spika alisema madiwani wanne ambao hawakuwepo walikuwa wamewaomba washirika wao bungeni wawapigie kura.
Madiwani 19 walikuwa bungeni wakati huo.
“Zaidi ya madiwani 23 walipiga kura kumwondoa Gavana Nyaribo mamlakani na hitaji la sheria la theluthi mbili limezingatiwa na kufikiwa,” akasema Spika Thaddeus Nyabaro.
Madiwani 23 waliopiga kura walitaja matumizi mabaya ya mamlaka na kukiuka katiba kama sababu za kufanya hivyo.
Hii ilikuwa mara ya tatu ambapo gavana alikuwa akikabiliwa na hoja ya kung’atuliwa madarakani baada ya majaribio mawili ya hapo awali kukosa kufaulu.
Hata hivyo, madai ya madiwani wanne sasa yanatia doa iwapo kweli idadi hitajika ya madiwani iliafikiwa kumbandua afisini.
Bunge la Kaunti ya Nyamira lina madiwani 35, jumla ya 20 wakiwa wale ambao walichaguliwa na 15 wakiwa madiwani wateule.
Wakati wa kutimuliwa kwa Bw Nyaribo, wadi tatu za Nyamaiya, Ekerenyo na Nyansiongo hazikuwa na wawakilishi na chaguzi ndogo za kuwapata madiwani wapya ziliandaliwa tu wiki jana.
Haya yakijiri, wakazi wa Nyamira wanasubiri kuona jinsi ambavyo Bunge la Seneti litashughulikia suala hilo. Gavana huyo amekuwa akikabiliana na madiwani na viongozi wengine waliochaguliwa.
Naibu wake Dkt James Gesami na Seneta Okongó Omogeni ni kati ya viongozi ambao wamekuwa wakitofautiana nao pakubwa.
Alichukua mamlaka kutoka kwa marehemu John Nyangarama na kwa wakati mmoja alifurushwa katika majengo ya bunge la kaunti akiwa naibu gavana.