Habari Mseto

Utata mahakamani gavana wa Wajir akihifadhi kiti

February 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Wajir Bw Mohammed Abdi Ijumaa aliponea chupuchupu kupoteza kiti chake huku uhitimu wake kimasomo ukiondolewa shaka.

Kukubaliwa kwa rufaa kulitamatisha kesi zinazotokana na uchaguzi mkuu wa Agosti 8 ,2017.

Utata mkali ulishamiri katika kesi hiyo iliyofanya Mahakama ya Juu kugawanyika majaji wanne wakiunga mkono ushindi wa Bw Abdi naye Jaji Mkuu David Maraga na Jaji Isaac Lenaola wakikubaliana na walalamishi Mabw Ahmed Abdullahi na Abdi Muhumed kwamba Gavana huyo hajahitimu kimasomo kuhudumu katika wadhifa huo.

Hata hivyo Bw Abdi ataendelea kuwa Gavana licha ya utata huo mkali wa masomo yake ukisalia kuwa suala nyeti.

Ushindi wa Bw Abdi ulihojiwa baada ya mkazi mmoja wa kaunti hiyo kuhoji masomo yake.

Mawakili Fred Ngatia, Tom Macharia na Nelson Havi walimtetea Bw Abdi wakisenma amehitimu huku mawakili wenye tajriba ya juu Mabw Ahmednassir Abdullahi , James Orengo na Omwanza Ombati wakisema hajahitimu kimasomo kuongoza kaunti hiyo.

Bw Orengo aliieleza mahakama hii hiyo kuidhinisha ushindi wa Bw Abdi ni sawa na kumtunuku shahada ya digirii.

Wakili Tom Macharia (kulia) aliyemwakilisha gavana Abdi. Picha/ Richard Munguti

Katika uamuzi huo uligawa Mahakama ya Juu pande mbili huku majaji wanne wakiunga mkono ushindi wa Bw Abdi wakisema “ suala la elimu yake iliimbuliwa katika Mahakama Kuu na wala sio mbele ya tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ambayo ingeliutatua na kuzuia uteuzi wake.”

Jaji Maraga na Jaji Lenaola walikubaliana kwa kauli moja na kusema Bw Abdi hakuhitimu kuwa Gavana kwa vile hana cheti cha Digirii.

Lakini Majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang , Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u walikosoa maamuzi ya Mahakama za Rufaa na Mahakama Kuu kwa kuchukulia suala hilo kwa uzito ilhali lilikuwa limepenya mlango wa uteuzi wa IEBC.

“Kama suala limeiponyoka IEBC iliyotunukiwa jukumu la kuwateua wawaniaji viti na mmoja kushinda basi kesi ikiwasilishwa mahakama kuu itakuwa imepotea njia,” alisema Jaji Smokin Wanjala aliyesoma uamuzi wa majaji wanne wenye maoni sawa kuhusu ushindi wa Bw Abdi.

CJ na Jaji Lenaola walikubaliana kwa kauli moja kuwa lazima sheria ifuatwe na wale waliotimiza masharti ya kuchaguliwa ndio wanaofaa kuwania nyadhifa za uchaguzi.

Jaji Mkuu (CJ) David Maraga-kulia- na Jaji Smokin Wanjala wasoma uamuzi wa kesi ya kupinga ushindi wa Bw Mohammed Abdi kuwa Gavana wa Wajir Picha/ Richard Munguti

Majaji hao wawili waliangazia kwa kina ushahidi tofauti tofauti Bw Abdi aliowasilisha katika hafla mbali mbali alipokuwa akiwania wadhifa wa Ubalozi na Ugavana..

Jaji Maraga aliyesoma maamuzi yake na Jaji Lenaola alisema Bw Abdi alieleza kamati ya bunge iliyomhoji akiwania Ubalozi kwamba hakuwa amehitimu kwa cheti cha digirii.

Lakini alipofika mbele ya kamati ya IEBC ya kuwateua wawaniaji viti alisema “ alikuwa amehitimu na shahada ya digirii katika somo la Biashara na digirii ya uzamili katika masuala ya ushirikiano wa kimataifa.”

“Ushahidi Bw Abdi aliowasilisha mbele ya hii mahakama kutoka chuo kikuu cha Kampala ulikuwa umetiwa saini na msajili wa chuo badala ya kutiwa saini na msimamizi wa kitivo katika chuo hicho,” walisema Majaji Maraga na Lenaola.

Majaji hao wawili walisema ni fedheha kwa sheria kutozingatiwa na kuidhinishwa kwa mwaniaji kiti asiyehitimu.

Majaji hao wawili walikubaliana maamuzi ya Mahakama kuu na Mahakama ya Rufaa kubatilisha matokeo ya ushindi wa Bw Abdi.

Wafuasi wa Bw Abdi nje ya mahakama ya juu Nairobi Februari 15, 2019. Picha/

Kwa upande wa majaji wanne waliotofautiana na CJ na Jaji Lenaola walisema kuwa suala la kuhitimu kimasomo kwa Bw Abdi lilipaswa kushughulikiwa na IEBC na wala sio mahakama kuu.

“Suala la kuhitimu kimasomo lilipasa kuamuliwa na majopo ya IEBC na ile ya kuamua mizozo ya vyama vya kisiasa almaarufu PDDT,” walisema Majaji Ibrahim, Ojwang, Wanjala na Ndung’u.

Lakini wafuasi wa Bw Abdi na wale wa Gavana wa zamani walitofautiana vikali nje ya mahakama nusra ya kioja kuzuka.