• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Utata wa wauaji kiwandani kuvaa sare za polisi

Utata wa wauaji kiwandani kuvaa sare za polisi

Na ERIC MATARA

UFICHUZI kwamba wauaji wa mfanyabiashara maarufu wa Nakuru, David Mwangi Wachira walikuwa wamevalia sare za polisi umeingiza utata katika uchunguzi kuhusu mauaji hayo.

Bw Wachira, 45, maarufu kama Kamleshi, ambaye alizikwa wikendi iliyopita, aliuawa kwa kuvamiwa na genge la watu katika kampuni yake ya Biscept Limited Company iliyoko eneo la Viwandani mjini Nakuru.

Picha za kamera ya CCTV ambazo Taifa Leo ilipata zinaonyesha kuwa mauaji hayo ya kinyama yalitekelezwa na wanaume sita waliovalia magwanda ya polisi.

Picha hizo zinawaonyesha wavamizi hao wakiingia ndani kampuni hiyo wakiwa na silaha mbalimbali zikiwemo nyundo na panga kabla ya kuamuru kila mtu alale chini.

Walifunga mikono na miguu ya wafanyakazi kabla ya kumuua Bw Mwangi.

Picha hizo za CCTV pia zinaonyesha wavamizi hao wakimgonga marehemu kichwani kwa nyundo mara kadha, kabla ya kuburuta mwili wake na kuuweka karibu na mahala ilipokuwa miili ya walinzi wake. Mikono na miguu ya Bw ilikuwa imefungwa kwa kamba.

Wauaji wengine wanaonekana wakipekua ofisi ya marehemu kana kwamba walikuwa wakitafuta vitu vya thamani kabla ya kuondoka kwa kuruka ua wa kiwanda hicho.

Hata hivyo wavamizi hao hawakuiba chochote katika kiwanda hicho, isipokuwa simu za Bw Mwangi.

Mnamo Jumanne, familia ya marehemu ilidai polisi wanajivuta kuwakamata washukiwa licha ya nyuso zao kuonekana kwenye picha za CCTV.

“Tangu mauaji ya Bw Mwangi wiki moja iliyopita, wauaji wake hawajakamatwa. Tunauliza ikiwa polisi wamejitolewa kuendesha uchunguzi au wanawalinda wenzao. Tumetamaushwa zaidi kwa sababu wavamizi hao walikuwa wamevalia sare za polisi,” akasema mmoja wa jamaa wa marehemu.

Kamanda wa Polisi wa Nakuru, Stephen Matu aliambia Taifa Leo kwamba wanafuatilia habari muhimu kuwawezesha kuwanasa wahusika.

“Tunaomba tupewe muda ili tuweze kufanya uchunguzi wa kina. Tutahakikisha kuwa wauaji hao wamekamatwa na kufikishwa kortini,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uchambuzi wa hadithi...

Washirika wa Ruto magharibi waonywa

adminleo