Habari Mseto

Utepetevu wa Wizara ya Afya wazidi kufichuka

December 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na NASIBO KABALE

WIZARA ya Afya (MoH) ilikosa kuwachukulia bima ya afya madaktari licha ya kupewa Sh576 milioni na Hazina Kuu.

Katibu wa Wizara ya Fedha Julius Muia, Alhamisi aliambia Kamati ya Seneti kuhusu Afya kuwa Hazina Kuu ya Kitaifa ilitenga fedha hizo katika mwaka wa fedha uliokamilika Juni.

Alisema hata baada ya kupewa pesa hizo, MoH ilikosa kupeleka fedha hizo kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Kitaifa (NHIF) ili kusaidia madaktari ambao hawakuwa na bima, na ikabidi pesa hizo zirudishwe Hazina Kuu.

“Fedha hizo zilikuwa zimeidhinishwa katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 lakini MoH ilikosa kuzitumia hivyo zikaelekezwa kwingineko,” akasema.

Dkt Muia alisema kuwa MoH haikutuma maombi mapya ya kutaka ipewe fedha hizo.

Lakini MoH ilijitetea kwa kusema kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti ya Wizara ya Afya mwishoni mwa mwezi wa Juni hivyo haikupata fursa ya kuzihamishia katika akaunti ya NHIF.

“Fedha hizo ziliwekwa katika akaunti za wizara mwishoni mwa Juni hivyo ilikuwa vigumu kuzihamishia katika akaunti ya NHIF,” akasema Dkt Mercy Mwangangi, Waziri Msaidizi wa Afya.

Dkt Mwangangi alisema kuwa wizara imeomba Sh520 milioni kutoka kwa Hazina Kuu ili kuzitumia kuwapa bima madaktari walioajiriwa kwa kandarasi.

Suala la wahudumu wa afya kukosa bima ya matibabu limeangaziwa zaidi tangu kuzuka kwa janga la corona ambapo baadhi yao wamekuwa na matatizo ya kupata matibabu kwa kukosa bima hiyo.

Kisa cha majuzi kilichoonyesha utepetevu wa MoH ni kifo cha Dkt Stephen Mogusu aliyeaga wiki hii kutokana na Covid-19 na hakuwa na bima ya matibabu.