Habari Mseto

Uteuzi wa Joho wafufua joto la kisiasa lililokuwa limesahaulika Pwani

Na WINNIE ATIENO July 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto alimaliza ziara yake eneo la Pwani kwa kujaribu kuzima joto la kisiasa kati ya viongozi wa chama chake tawala cha UDA na wale wa upinzani, ambalo lilizuka upya baada ya kumteua Naibu Kinara wa ODM, Bw Hassan Joho kama waziri.

Rais ambaye aliandamana na wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza wakiwemo Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Hassan Omar, mwenzake wa Nyali Mohammed Ali na wengineo, aliwarai viongozi hao kufanya kazi kwa karibu na wenzao wa upinzani ambao amewateua kwenye baraza lake la mawaziri.

Dkt Ruto aliweka wazi kuwa hakuna mbabe wa kisiasa katika chama chake tawala cha UDA eneo la Pwani, kufuatia mzozo ambao umekithiri kati ya Bw Omar na Bw Ali.

Ubabe na uhasama wa kisiasa kati ya Bw Ali na Bw Omar umekithiri kwa muda sasa hasa ikikisiwa kuwa wawili hao wanaazimia kuwania ugavana wa Mombasa.

Chama cha UDA kimejaribu kusuluhisha joto hilo la kisiasa bila mafanikio. Hata hivyo, kuingia kwa Bw Joho serikalini huenda kukaongeza uhasama huo huku ikikisiwa mwanasiasa huyo ambaye ni kigogo wa siasa atazima ndoto za wanasiasa wa Pwani kufuatia umaarufu wake, utajiri na ufuasi mkubwa alionao.

Rais Ruto aliwataka viongozi wote wa Mombasa kumakinikia uongozi bora na kutumikia wananchi.Dkt Ruto alisema hayo kufuatia cheche za kupigania tiketi ya chama cha UDA katika uchaguzi wa ugavana wa 2027 baina ya Bw Ali na mwenzake Omar.

Gavana wa sasa Bw Abdulswamad Nassir pia anapania kugombea kiti chake.“Nimeshuhudia ubabe wa kisiasa lakini naomba tudumishe amani, tushirikiane na tufanye kazi pamoja badala ya kuangalia umaarufu wa wanasiasa. Naomba viongozi wadumishe siasa za amani na tuunganishe wakazi,” aliongeza.

Aliwatata wabunge Bw Omar, na Bw Ali, na viongozi wengine wa UDA kuweka tofauti zao za kisi Wakenya kazi.“Ni wapigakura ambao wataamua nani atakuwa mjumbe wao, diwani, Gavana, Seneta na Rais,” alisema Rais.

Hata hivyo, Bw Ali, alisema licha ya kuwa wamewakaribisha wanasiasa wa ODM serikalini, wanafaa kuwatumikia Wakenya wote kazini.

“Tumemkaribisha Bw Joho, lakini asifanyie wakazi wa Mombasa kazi bali Wakenya wote. Wakazi wa Mombasa wanalia sababu ya uongozi mbaya ambao hauna maendeleo. Nitaendelea kutathmini utendakazi wa serikali ya kaunti,” alisema Bw Ali.

Alisema hatanyamaza akiangalia uongozi mbaya ukiendelezwa Mombasa.Bw Ali ambaye anahudumu kama Mbunge wa Nyali kwa muhula wa pili alimtaka Rais kutoingilia siasa za Mombasa na awachane na viongozi hao kumenyana.

“Wakazi wa Mombasa wameteseka sana hasa katika swala la maendeleo. Uongozi ulioko umeshindwa kuwajibika, ni miaka miwili tangu wachukue hatamu lakini hakuna maendeleo yoyote,” alisema Bw Ali.

Alisema Bw Nassir ameshindwa kuleta maendeleo hata kujenga choo cha umma ilhali ameweza kujenga shule za umma.Alisema yuko tayari kumenyana na Gavana Nassir, Bw Omar, na Bw Joho kisiasa.

Hata hivyo, Bw Omar, alisema viongozi wa UDA wanafaa kuacha uhasama wa kisiasa na kujipiga kifua na badala yake kushirikiana.