• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:30 PM
Uteuzi wa Mutyambai ulitokana na urafiki wangu na Uhuru – Kalonzo

Uteuzi wa Mutyambai ulitokana na urafiki wangu na Uhuru – Kalonzo

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema kuwa uteuzi wa Bw Hilary Mutyambai kuwa Insepekta Jenerali wa Polisi (IG) ulitokana na uhusiano wa karibu kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Akiongea katika hafla moja ya maadhimisho ya siku ya harusi ya Askofu Gerans Manzi na Queen Rhoda katika eneo la Kauma, eneo bunge la Kitui Magharibi, Bw Musyoka aliwataka wafuasi wake na jamii ya Wakamba kwa jumla kuunga mkono uteuzi huo.

“Utuezi wa ndugu yetu Muytambai ni matunda ya kuimarika kwa uhusiano kati yangu na Mheshimiwa Rais Kenyatta. Niliposema kuwa nitafanya kazi na Rais kiasi cha kuwa mtu wake wa mkono wangine walionekana kukerwa. Lakini sasa matokeo yake imekuwa uteuzi wa mtu kutoka Ukambani kuwa Inspekta Jenerali wa polisi,” akasema Bw Musyoka.

Bw Mutyambai ambaye ni afisa wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) anatoka eneo la Masii, katika kaunti ya Machakos, ambayo ni ngome ya kisiasa ya Bw Musyoka.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Wiper ambaye alikuwa ameandamana na Seneta wa Kitui Enock Wambua na Afisi Mkuu wa Bodi ya Kuainisha Filamu Nchini (KFCB) Dkt Ezekiel Mutua aliwahakikisha wafuasi wake kuwa bado yuko katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuuu wa 2022.

“Watu wengi walisema kuwa hatua yangu ya kufanya kazi na Uhuru yaashiria kwamba nimejiondoa kutoka kinyang’anyiro cha urais. Ningependa kukariri kwamba sijabadili azma yangu ya kuwa debeni 2022,” akasema.

Licha ya Bw Musyoka kudai kushawishi uteuzi wa Bw Mutyambai, duru kutoka idara ya usalama inasema kuwa jina la jasusi huyo pamoja na watu wengine watatu iliwasilishwa kwa Rais Kenyatta na Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC).

Itakumbukwa kuwa wakati wa mazishi wa babake marehemu Mzee Peter Musyoka Mairu, Agosti mwaka jana, kiongozi huyo wa Wiper alitangaza kuwa atakuwa “mtu wa mkono” wa Rais Kenyatta na kuwaonya wafuasi wake dhidi ya kumuuliza swali lolote kuhusu uamuzi huo.

Tamko hilo lilimkera aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Wiper Profesa Kivutha Kibwana aliyesema lilidunisha sio tu Bw Musyoka kama mtu binafsi jamii ya Wakamba na wafuasi wake kwa jumla.

“Kalonzo ni kiongozi mwenye hadhi ya juu ambaye hapaswi kutoa tamko kama hilo la kudunisha,” akasema Profesa Kibwana ambaye pia ndiye Gavana wa Makueni.

Hiyo ndio ilikuwa mwanzo wa uhasama kati ya viongozi hao wawili hali iliyopelekea Profesa Kibwana kuondolewa kama mwenyekiti wa chama hicho.

You can share this post!

Unilever yajikakamua kupenya kwa soko la dawa ya meno

Jina langu liondolewe kwa ripoti ya PAC – Monica Juma

adminleo