• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 2:58 PM
‘Uzinzi, salamu za mikono vinahujumu vita dhidi ya Covid-19’

‘Uzinzi, salamu za mikono vinahujumu vita dhidi ya Covid-19’

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amewasihi wakazi wa jiji hilo waepuke kuamkuana kwa mkono, aghalabu kwa wakati huu, ili kupunguza kuambukizana virusi vya corona.

Bw Joho alisema salamu za mkono zinafaa kuepukwa wakati huu wa janga la corona licha ya kwamba ni za kuonyesha staha miongoni mwa wanajamii.

Kadhalika kiongozi huyo aliwaonya wanaozini akiwapa nasaha wakome. Alisema kuwa na ‘mipango mingi’ ni hatari wakati huu Kenya inakabiliana na janga la corona.

Akiongea alipokuwa akizindua mradi wa maji huko Tudor, Bw Joho aliwataka wakazi kufuata kanuni za Wizara ya Afya ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Kanuni hizo ni pamoja na kuosha mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa na kutotangamana na watu kwenye umati.

Alisikitishwa na tabia ya vijana kupuuza kanuni na kuambukiza jamaa zao hivyo basi kuweka maisha ya wale wenye magonjwa kama kisukari, saratani, presha na hata matatizo ya kiumri kwa wazee, kwenye hatari ya kuangamizwa na virusi vya corona.

“Ukiambukiza jamaa yako utaishi na majuto milele. Vijana, tafadhalini tuwalinde wazee na jamii zetu; tuache kutangamana ovyo na kubeba virusi kila mahali. Corona iko na bado tuko kwenye hatari. Nasikitishwa kila ninapoona watu wakiamkuana kwa mikono licha ya hatari ya kuambukizana virusi vya corona. Lazima tukubali maisha yetu yamebadilika. Hatuwezi kuishi kana kwamba hakuna corona,” alisihi.

You can share this post!

TANZIA: Mchezaji Ian Waraba wa Kenya Harlequins afariki...

Trump aondolewa katika ukumbi mmojawapo ufyatulianaji...

adminleo