Vaeni nguo zenye joto mwilini – Serikali
CHARLES WASONGA Na SAMMY WAWERU
Watu wameshauriwa kuhakikisha wanavalia mavazi mazito msimu huu wa baridi ili kupunguza athari za virusi vya corona (Covid-19).
Wizara ya Afya imesema baridi kali na ambayo imekuwa ikishuhudiwa maeneo mbalimbali nchini kuanzia Julai 2020, hasa kaunti ya Nairobi, Kiambu na Nyeri, ni hatari kwa wenye matatizo ya baridi na pia walioambukizwa corona.
“Taifa limekuwa likishuhudia msimu wa baridi tangu mwezi Juni na inatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa Agosti 2020. Inazua hatari kwa watu wetu haswa watoto na wenye matatizo ya mapafu na maradhi hatari kama vile Pumu (Asthma),” akaonya Dkt Rashid Aman, Waziri Msaidizi katika Wizara.
Alisema baridi kali inayoendelea kushuhudiwa inachangia ongezeko la athari za mapafu, na ni hatari kwa walioambukizwa Covid-19, ikizingatiwa kuwa ni homa inayoathiri mapafu na viungo vingine muhimu mwilini katika kupumua.
“Ninahimiza watu wavalie mavazi mazito na yanayoongeza joto mwilini. Watu wajitahadhari hasa msimu huu wa baridi. Wenye mazoea ya kuvuta sigara na wanaugua Pumu, wakome,” Dkt Aman akasema.
Waziri alisisitiza haja ya kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake, uvaliaji maski na pia unywaji na ulaji wa vyakula moto msimu huu.
Alihimiza wenye historia ya maradhi hatari kuhakikisha wanatilia maanani matibabu waliyopendekezewa na madaktari, ili kudhibiti athari za magonjwa wanayougua.
“Ugonjwa wa kifua kikuu (TB) husambaa kwa kasi zaidi katika hali ya baridi na mahala ambapo pana msongamano wa watu. Hali hii pia huchangiwa na ukosefu wa vitamin D, mazoezi ya viungo na kupungua kwa kinga za mwili,” akaongeza.
Dkt Aman pia alisema wakati huu wa baridi watu wengi hupenda kujikusanya mahala pamoja, hali ambayo huongeza uwezekana wa virusi vya corona kuenea kwa haraka kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
“Wengine pia hukongamana pamoja baada ya kuanzisha moto ili kupasha miili yao joto,” akaongeza Waziri huyo msaidizi wa Afya.
Dkt Aman pia alionya kuwa japo ni muhimu watu kuota moto ili miili yao ipate joto, wanafaa kujiepusha na maeneo yenye moshi mwingi ili wasipate ugonjwa wa pumu.
“Nyumba zisizo na madirisha na malango mapana ya kuleta hewa safi pia yanaweza kuongeza uwezekano wa watu kuambukizwa magonjwa ya TB, Influenza na Covid-19,” akaeleza.
Kwa hivyo, waziri huyo msaidizi aliwataka Wakenya kuwa waangalifu msimu huu wa baridi kwa kuzingatia mikakati ya kukinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa hatari.
Dkt Aman pia aliwahimiza Wakenya kunywa maji kwa wingi msimu huu ili kuimarisha kinga ya miili yao.