Habari Mseto

Mshubiri kwa Valentino Dei ya OCS wa zamani kuhukumiwa kunyongwa

February 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

ILIKUWA Valentino Dei ya mshubiri kwa aliyekuwa Afisa mkuu wa Kituo cha Polisi cha Ruaraka (OCS) aliposimama wima kizimbani kwa huzuni baada ya kuhukumiwa kunyongwa kwa hatia ya kumuua mahabusu ndani ya seli miaka mitano iliyopita.

Bw Nahashon Muchiri Mutua (pichani), aliyemtazama Jaji Stellah Mutuku akisoma uamuzi wake, aliinamisha kichwa na hkuepuka kuwatazama kamwe watu wa familia yake waliojishika tama kusikia atatiwa kitanzi.

Pia mshtakiwa hakuangalia pale watu wa familia ya Martin Koome mahabusu aliyeshtakiwa kumuua walipokuwa wameketi kwa sababu ya fedheha.

Afisa huyo wa zamani wa polisi alipatikana na hatia ya kumuua Koome mnamo Desemba 19, 2013 ndani ya seli kituo cha Polisi cha Ruaraka.

Baada ya kuhukumiwa na kujulishwa kwamba anaweza kukata rufaa katika muda wa siku 14, Bw Mutua mwenye umri wa miaka 40 na baba wa watoto sita alijipa moyo na kuomba dhamana aliyokuwa ameweka mahakamani irudishiwe watu wa familia yake.

“Naomba dhamana niliyokuwa nimeweka hapa kortini nifanye kesi nikiwa nje irudishiwe watu wangu kwa vile sasa naenda kuanza maisha mapya ya mfungwa,” alisema Bw Mutua.

Jaji Stellah Mutuku akisoma uamuzi. Picha/ Richard Munguti

Alipokuwa anajitetea, Bw Mutua alighairi kitendo hicho cha mauaji ya Koome na kuwaomba watu wake msamaha licha ya kudumisha hakuhusika na kifo cha mahabusu huyo.

Lakini Jaji Mutuku alitupilia mbali ushahidi wake mshtakiwa na kusema “ndiye alihusika na kifo cha Koome.”

Koome alipata kichapo cha mbwa n ahata mahabusu mwingine alishikwa na kushtakiwa kisha akaachiliwa huru ndipo Mutua akashikwa na kushtakiwa.

Mshtakiwa alisema hata yeye ni mhasiriwa wa kitendo hicho kwa vile amepoteza kazi na sasa atatenganishwa na jamii yake.

“Kazi yangu ilikatizwa licha ya bidii niliyoweka hata nikapandishwa madaraka na kuwa Inspekta nikusimamia kituo cha Ruaraka,” Mutua alisema.

Mshtakiwa huyo alimweleza Jaji Mutuku kwamba alikuwa amehitimu kupandishwa cheo hadi Suparitendi kabla ya mkosi huo kumkumba.

Lakini Jaji Mutuku alisema ushahidi uliowasilishwa ulibaini kwamba kupelekwa kwa Bw Mutua kaunti ya Machakos ilikuwa njama ya kukwepa haki kutendeka katika kisa hicho cha mauaji kinyama ya mahabusu Koome.

Akitoa uamuzi Jaji Mutuku alikataa ombi la Bw Mutua kesi hiyo ichunguzwe tena kwa vile alidumisha hakumuua Koome na hakuwa na hatia.

Mkewe marehemu Martin Koome (mwenye kofia) akiwa nje ya mahakama ya Milimani, Nairobi Februari 14, 2018. Picha/ Richard Munguti

Jaji huyo alisema fursa ile iliyoko sasa kwa Bw Mutua ni kukata rufaa kupinga adhabu ya kifo aliyopitisha dhidi yake.

“Fursa iliyoko kwako sasa ni kukata rufaa ikiwa hukuridhishwa na uamuzi wangu,” Jaji Mutuku alimweleza mshtakiwa.

Jaji huyo alisema kesi hiyo ilichunguzwa barabara na ushahidi uliowasilishwa ulimuhusisha moja kwa moja na mauaji ya Koome.

Jaji Mutuku alisema adhabu ya kifo tu ndiyo inastahili ipitishwe dhidi ya afisa huyu wa polisi aliyekaidi majukumu yake ya kulinda maisha ya wananchi na badala yake akayatwaa maisha ya Koome.

“Nikitilia maanani jinsi Koome alivyokumbana na mauti akiwa mikononi mwa afisa wa usalama aliyetunukiwa jukumu ya kulinda maisha ya wananchi hii mahakama haina budi ila kupitisha adhabu ya kifo dhidi ya mshtakiwa,” alisema Jaji Mutuku.

Jaji huyo alisema Koome alitendewa unyama, kaumizwa, katiwa vidonda na hatimaye akauawa akiwa ndani ya seli.

“Adhabu ya kifo tu ndiyo inafaa ndipo iwe funzo kwa maafisa wengine wa usalama walio na tabia ya kupuuza maisha ya wananchi,” alisema Jaji Mutuku.