• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Vibanda vyachomwa mzozo kuhusu mji wa Keroka ukichacha

Vibanda vyachomwa mzozo kuhusu mji wa Keroka ukichacha

NA WYCLIFFE NYABERI

HALI ya sintofahamu inazidi katika mji wa Keroka unaozozaniwa na kaunti za Kisii na Nyamira baada ya vibanda vya wafanyabiashara kuteketezwa na watu wasiojulikana Jumatano usiku.

Mali ya mamilioni ya pesa iliharibiwa wakati wa kisa hicho kilichotekelezwa na watu wasiojulikana.

Kaunti hizo mbili zimekuwa zikizozania mji huo wa mpakani unaokua kwa kasi kuhusu ukusanyaji ushuru na kodi zingine.

Kila kaunti inadai kumiliki sehemu kubwa ya mji huo na maafisa wa kutekeleza amri za kaunti kutoka kila upande, wamekuwa wakigongana wanapofanya kazi yao.

Huku mzozo huo ukiwa kortini, hali ya kawaida bado haijarejea ilivyokuwa awali kabla ya kesi ya kwanza kuwasilishwa.

Mji huo wa Keroka umegawanywa katikati na barabara kuu ya Kisii-Sotik.

Sehemu zilizo juu ya barabara hiyo zimekuwa zikihesabiwa kuwa Nyamira na zile za chini zikihesabiwa kuwa Kisii.

Hivyo basi, tangu ujio wa ugatuzi, kaunti hizo zimekuwa zikikusanya kodi kuzingatia mpaka wa barabara hadi pale diwani wa Rigoma, Nyambega Gisesa alipoelekea mahakamani na kusema sehemu zingine zilizokuwa zikihesabiwa Kisii, zilikuwa upande wa Nyamira.

Aliwasilisha kesi yake mbele ya Jaji Mugo Kamau, wa masuala ya Ardhi na Mazingira.

Jaji huyo alitumia ripoti ya pamoja ya masoroveya kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na wale wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kutoa uamuzi wake.

Ilibainika katika ramani za taasisi hizo kuwa sehemu zingine zilizokuwa Kisii ziko Nyamira.

Kwa kutofurahia uamuzi huo, mawakili wa kuitetea serikali ya Kisii walikata rufaa kuhusu uamuzi wa Jaji Mugo wa Mahakama Kuu.

Lakini kabla ya kesi hiyo kusikizwa, uharibifu wa mali umeanza kutokea.

“Mimi ni muuzaji wa machungwa. Yameteketezwa yote. Hapa ndipo ninapotegemea kuikimu familia yangu. Sijui nitakapoenda sasa baada ya watu hao kunichomea kibanda changu na mali yangu yote,” Bi Rachael Bosibori ambaye ni mfanyabiashara katika sehemu ya Kisii, ambayo iliathrika pakubwa akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Mbolea feki NCPB ni ithibati tosha walaghai wameteka nyara...

EACC yaondolea Chiloba kesi ya ufisadi iliyopelekea...

T L