Vifo kutokana na ajali vyaongezeka
Na PETER MBURU
IDADI ya vifo kutokana na ajali tangu mwaka ulipoanza hadi Mei 4 imeongezeka mwaka huu, ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka uliopita.
Kulingana na takwimu za idara ya trafiki nchini, ajali zilizosababisha vifo katika miezi hiyo minne mwaka huu ni 967, ikilinganishwa na ajali 847 katika kipindi sawa mwaka uliopita.
Takwimu hizo aidha zinaonyesha kuwa katika kipindi hicho, mwaka huu watu 1157 wamepoteza maisha yao, idadi ya juu ikilinganishwa na watu 1056 waliofariki katika ajali za barabarani kipindi hicho mwaka jana.
Takwimu hizo aidha zinaonyesha kuwa katika kila kitengo cha ajali vikiwa cha wapita njia, waendeshaji baiskeli na pikipiki, madereva na wasafiri katika magari, idadi ya watu waliokufa mwaka huu imeongezeka.
Takwimu hizi zilitolewa, wakati Tume ya Kuimarisha Usalama Barabarani (NTSA) ilianzisha rasmi kampeni ya siku sita kuhusu usalama wa barabarani katika Ukumbi wa Makongamano ya Kimataifa wa Kenyatta (KICC), ambayo inaendeshwa kote duniani, kuhamasisha kuhusu usalama wa barabarani na kulinda maisha.
Tume hiyo, hata hivyo, ilipongeza sekta ya magari ya usafiri wa umma kwa kudumisha sheria za trafiki msimu wa pasaka mwezi uliopita, ikisema kuwa hakukushuhudiwa kifo kutokana na ajali za magari hayo, kama jinsi imekuwa miaka ya mbeleni.
“Hiyo ilikuwa hatua nzuri na ambayo inaonyesha kuwa tunaweza kudumisha usalama barabarani na sote kusafiri na kufika tunakoenda bila matatizo,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa NTSA Francis Meja.
Japo akitaja tatizo la ajali za barabarani kuwa changamoto kote ulimwenguni, Bw Meja alisema hali ya madereva kuendesha magari kwa utepetevu nchini ndiyo imesababisha kushuhudiwa kwa ajali nyingi mara kwa mara.
“Sote tunaonekana kuwa na haraka, na si haraka ya kwenda popote na mambo madogo ambayo tunapuuza ndiyo yanaishia kusababisha ajali na vifo. Sharti tubadili tabia,” akasema Bw Meja.
Katika ajali za pikipiki, watu 223 wamefariki mwaka huu ikilinganishwa na watu 205 hadi Mei 4 mwaka jana, nayo idadi ya waliojeruhiwa vibaya ikipanda kutoka 186 hadi 385, asilimia 107.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Julius Kanampiu alisema kuwa polisi wataanza kuwinda wasiofuata sheria za trafiki punde ilani ambayo NTSA ilitoa kwa shule za kutoa mafunzo na wahudumu ikifikia mwisho.