Vijana Kiambu kunufaika chini ya mpango wa kuwawezesha
Na LAWRENCE ONGARO
MRADI wa vijana wa Youth Empowerment Programme Kaunti ya Kiambu ulizinduliwa mjini Ruiru kwa lengo la kuinua vijana.
Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu katika Bunge la Kitaifa, Bi Gathoni Wa Muchomba alizindua mradi huo Ijumaa, mgeni wa heshima kwenye hafla hiyo akiwa Waziri wa Maswala ya Umma, Vijana na Jinsia, Profesa Margaret Kobia.
Wahudumu wa bodaboda wapatao 400 walifuzu kwa mafunzo ya uendeshaji pikipiki, huku wakikabidhiwa kofia za kuvalia wakiwa kazini.
Vikundi vingine vilivyonufaika na vifaa vya kujiendeleza ni wanawake wakongwe, walemavu, wasusi, wanafunzi wa ngumbaru na wanasoka kutoka Juja.
Bi Wa Muchomba alisema kila mmoja anastahili kujitahidi ili kujiendeleza zaidi.
“Ninataka kuona kila mmoja akifanya juhudi ili kujiendeleza. Yote haya mnayoshuhudia ni kwa sababu ya mpango wa serikali wa ajenda nne muhimu,” alisema Bi Wa Muchomba.
Bidii
Prof Kobia aliyekuwa mgeni wa heshima aliwashauri watu wote walionufaika na mpango huo kuwa mstari wa mbele na kufanya bidii.
“Sisi kama mawaziri tuliarifiwa na Rais Uhuru Kenyatta tufanye juhudi kuzuru mashinani ili kuelewa matatizo anayopitia mwananchi,” alisema Prof Kobia.
Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara aliwahimiza wananchi wasikubali kuingizwa kwa siasa duni kwani viongozi waliochaguliwa wanastahili kufanyia mwananchi kazi.
“Iwapo tutazingatia ajenda nne za serikali, bila shaka serikali itaafikia malengo yake muhimu,” King’ara alijulisha umati.
Alisema chuo cha kiufundi kitafunguliwa hivi karibuni mjini Ruiru ambapo wanafunzi watasomea huko bure bila kulipia karo.
“Siku hizi kazi za kiufundi zimechukua nafasi ya kwanza kwa sababu zimepiku zile za ofisini,” alielezea Bw King’ ara.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi kadha kama Bi Esther Passaris (Nairobi), Bi Milly Odhiambo (Suba Kaskazini), Bi Pamela Odhiambo (Migori), na Bw Anthony Oluoch (Mathare).
Bi Passaris alipendekeza wanawake waheshimiwe kwa kupewa haki yao uongozini.
“Sisi tunataka ugavi wa mamlaka sare ya asilimia 50. Hiyo itafanya wanawake kuwa katika uongozo kamili.
Bi Milly Odhiambo aliwataka Wakenya wakumbatie nafasi nzuri ya ‘Handisheki’ ya Uhuru na Raila Odinga.
Bi Pamela Odhiambo wa Migori, aliwashauri wananchi kuwachagua viongozi wenye maono watakaoleta maendeleo nchini bila ukabila.