• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Vijana wahamasishwe badala ya kutumiwa vibaya – mbunge

Vijana wahamasishwe badala ya kutumiwa vibaya – mbunge

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwahamasisha vijana kwa kuwaonyesha mambo na shughuli muhimu badala ya kuwatumia vibaya, amesema mbunge.

Mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina amewashutumu viongozi wachache wanaowatumia vibaya vijana kwa manufaa yao wenyewe.

“Ninawalaumu viongozi wanaotumia njia isiyo njema ya kuwapatia hela kiasi vijana ili watende maovu. Serikali inastahili kuwachukulia hatua kali viongozi hao bila huruma,” alisema mbunge Wainaina.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano alipokutana na vikundi 200 vya wahudumu katika sekta ya bodaboda kwa lengo la kuwahamasisha kujihusisha na mpango wa J-Hela.

Alisema katika mpango huo wa J-Hela wanaweza wakaweka fedha zao pale halafu baadaye wanachukua mikopo mara tatu ya akiba walioweka.

“Lengo langu kuu la kufanya mkutano na wahudumu hawa wa bodaboda ni kuwapa mwongozo wa jinsi wanavyoweza kuboresha maisha yao bila kupata shida,” alisema Bw Wainaina.

Aliwahimiza kujiweka kwa vikundi ili waweze kufanya miradi ya kuwainua kimaisha.

Alishutumu kitendo cha kufedhehesha cha Jumapili ambapo ghasia zilishuhudiwa Kenol, Kaunti ya Murang’a.

“Ni masikitiko makubwa kupata ya kwamba vijana hao wadogo wanatoka katika kijiji duni cha Kiandutu kilichoko Thika,” alisema mbunge huyo.

Alitaka serikali kukabiliana vilivyo na viongozi wanaowatumia vibaya vijana hao kwa manufaa yao wenyewe.

Aliwashauri wazazi pia wawe mstari wa mbele kuwashauri wana wao kila mara kujiepusha na viongozi ambao nia yao ni kuwatumia vibaya.

Alipongeza mpango wa serikali wa kuwapa ajira vijana zaidi ya 200,000 kote nchini.

Alisema mji wa Thika kuliajiriwa vijana wapatao 700 jambo alilosema ni hatua nzuri kwa maisha yao.

Alishauri chama tawala cha Jubilee kiite viongozi wake pamoja ili kutatua tofauti zao kabla ya mambo kuharibika.

“Migawanyiko inayoshuhudiwa katika chama hicho ni taswira mbaya kwa wafuasi wake na wananchi kwa jumla,” alisema Bw Wainaina.

Alisema miaka miwili iliyosalia ni ya kumpa Rais Uhuru Kenyatta fursa kukamilisha baadhi ya miradi aliyoahidi wananchi badala ya kuingilia kampeni za mapema za mwaka wa 2022.

  • Tags

You can share this post!

Kizungumkuti cha Oezil baada ya Arsenal kumtema kwenye...

Westgate: Korti kuhukumu wawili