Vijana wataka wabunge wapunguziwe malipo
Na OSCAR KAKAI
MUUNGANO wa vijana umeitaka serikali kupunguza marupurupu ya wabunge, maseneta na madiwani pamoja na kupunguza idadi ya walioteuliwa katika mabunge ya kaunti nchini kama njia moja ya kupunguza gharama ya mishahara kwa wafanyikazi wa serikali na kutatua shida za kifedha zinazokumba nchi.
Akiongea na Taifa Leo mjini Kapenguria, Mwenyekiti wa kitaifa wa muungano wa Youth Bunge Forum nchini, Bw Richard Ruto Todosia, alisema inashangaza kwa nini wabunge, maseneta na madiwani wanapata marupurupu ya juu hata wanapohudhuria vikao vya bunge ilhali hiyo ni kazi wanayolipwa kufanya.
“Hatuelewi mbona watu hawa wanapewa marupurupu ilhali wako kazi ya kawaida,” akasema.
Alipinga hatua ya serikali ya kuwatoza Wakenya ushuru wa juu na akapendekeza kuwepo mbinu mwafaka za kupanua uchumi ili kuongeza uzalishaji mali na nafasi za kazi.
Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa idadi ya viongozi nchini ni kubwa kupita kiasi.
“Tunawakilishwa na idadi kubwa na wengine hawana kazi ya kufanya,” akasema.
Msimamo wake uliungwa mkono na Katibu wa Baraza la Kitaifa la Vijana, Bw Thomas Kalya.
Bw Todosia anapendekeza kuwa ni vyema kuwe na mswada wa kuwaondoa viongozi ambao hawana kazi ya kufanya.
Aliwataka viongozi nchini wakome kuwa walafi wa kutaka kulipwa pesa kupita kiasi.
“Kuna watu wanalipwa chini ya shilingi elfu kumi na wengine wanapaya marupurupu ya elfu kumi kwa masaa chache,”alisema.