Habari Mseto

Vijiji Baringo vyaanza kushuhudia utulivu

June 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FLORAH KOECH

HALI ya utulivu imeanza kurejea katika vijiji vilivyokumbwa na machafuko Baringo Kaskazini.

Hii ni kutokana na uwepo wa maafisa wa usalama waliopiga kambi katika maeneo yanayoshukiwa kuwa maficho ya wahalifu wenye silaha.

Wahalifu hao wamesababisha vifo vya watu wengi na kuwafanya baadhi ya wakazi kuhama makazi yao huku wengine wakipoteza mifugo.

Maelfu ya watu walitoroka vijiji vya mpakani kutokana na mashambulio ya mara kwa mara huku wengine wakiachwa bila makao tangu mwanzoni mwa mwaka baada ya majangili kuvamia maeneo hayo yakiwemo Kagir, Kibenos, Koroto, Kiboino, Rormoch, Kosile, Ng’aratuko, Sangorok, Yatya, Namba, Koibaware, Sibilo, Chemoe, Chepkewel, Kapsebeiwa, Naiben, Koibaisa, Nyalilbuch, Kapsoi, Chelelyo na Kiplelchony.

Kutokana na hali hiyo, masomo yalikwama katika baadhi ya shule zikiwemo shule za msingi za Yatya, Kagir, Kosile, Kibenos, Sibilo, Koroto, Biretwonin, Akoreyan, Moinonin, Chepkewel, Rondinin, Karimo, Sesianin, Kapsepeiwa na Naipen.

Kulingana na takwimu za serikali, zaidi ya watu 10,000 katika eneo hilo walihamishwa kufuatia tishio la ukosefu wa usalama, na maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Barketiew, Loruk, Sibilo na Rondinin.

Huko Baringo Kaskazini pekee, zaidi ya watu 18 waliuawa kwa kupigwa risasi na majangili, huku wengine wengi wakiuguza majeraha ya risasi tangu mwanzoni mwa mwaka.

Hata hivyo, wakazi katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa wameanza kufanya shughuli zao za kawaida, tofauti na hali ilivyokuwa miezi kadhaa iliyopita ambapo wahalifu wenye silaha walisababisha uharibifu mkubwa katika maeneo kadhaa na kuua watu wakiwemo maafisa wa usalama waliotumwa kurejesha amani.

Bw Richard Chepchomei mkazi wa eneo hilo, alisema kwa sasa hali ya utulivu imeanza kushuhudiwa lakini anasema kwamba wahalifu waliojihami wanaofanya uharibifu katika eneo hilo kwa kuiba mifugo kutoka kwa jamii jirani na kuua watu wanapaswa kuondolewa.

“Serikali inafaa kuwatuma maafisa zaidi ili kuimarisha usalama. Kwa muda wa wiki mbili zilizopita, utulivu umeanza kurejea katika vijiji vya mpakani na pia tunatoa wito kwa maafisa wa usalama kuimarisha doria ili kuwaepusha wavamizi na kuruhusu watu waanze maisha yao ya kawaida,” akasema Bw Chepchomei.

“Ni vizuri amani inarejea polepole katika eneo . Tumekuwa tukipoteza maendeleo kutokana na ukosefu wa usalama katika eneo letu. Operesheni ya usalama ya kuwaondoa majambazi hatimaye inazaa matunda,” alisema Bi Grace Chebii kutoka kijiji cha Ng’aratuko kinachokabiliwa na ukosefu wa usalama.

Kamanda wa Kaunti ya Baringo, Bw Julius Kiragu, alidokeza kuwa ili kuwahakikishia wenyeji usalama wao, wameanzisha vitengo katika vijiji ili kuzima mashambulio yanayolenga maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama.