Habari Mseto

Vikwazo katika biashara ya nyama vyawekwa eneo la Kati

May 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

KAMATI ya kiusalama eneo la Kati imeweka vikwazo vya uchinjaji mifugo na usafirishaji wa nyama na kisha kuahidi misako mikali katika sekta hiyo huku vita dhidi ya wizi wa mifugo vikiendelezwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Wilfred Nyagwanga na ambaye pia ni mshirikishi wa masuala ya kiusalama eneo hilo ameambia Taifa Leo kuwa vikwazo hivi vilianza kutekelezwa Mei 5, 2019, na vitaendelea hadi atangaze kukomeshwa kwavyo.

“Hii ni baada ya eneo hili kukumbwa na visa vingi kila kuchao vya mifugo kuibwa na kisha uchunguzi wetu kubaini kuwa biashara ya nyama haramu ndiyo kiini cha wizi huu,” akasema Nyagwanga.

Alisema kuwa Kaunti ambazo zimeathirika zaidi katika visa hivi ni Nyandarua, Kiambu, Nyeri, Murang’a na Kirinyaga.

“Tumebaini kuwa magenge ya vijana wanaoshirikiana na wafanyabiashara wasio na adabu za kismingi kuhusu uadilifu ndio wanashirikisha kashfa hii na hivyo basi kutupa sababu ya kujibu kimikakati kupitia uzinduzi wa vikwazo kadhaa,” akasema.

Alisema kuwa magenge hayo baada ya kuiba mifugo hao huchinjia katika vichaka usiku na kisha kutumia uchukuzi wa barabarani kuingiza nyama ya wizi sokoni.

Katika hali hiyo, alisema kuwa wahudumu wa vichinjio ambao watanaswa katika eneo hilo wakichinja mifugo yao usiku watakamatwa na kushtakiwa.

“Hatutaki mifugo kuchinjwa usiku. Muda wa kuchinja katika hali hii ya vikwazo ni kuanzia saa kumi na moja (11) asubuhi hadi saa 12 jioni. Uchinjaji mwingine wowote wa mifugo katika harakati za kibiashara ni haramu,” akasema.

Alisema kuwa nao wauzaji katika maduka ya nyama watahitajika kuwa na ushahidi wa walikponunua nyama zao, ziwe na muhuri wa ukaguzi kuhusu ufaafu wa matumizi ya binadamu nka wasiwe nao pia wakisafirisha nyama usiku.

Aidha, alisema kuwa maafisa wa kiusalama wameelekezwa wawe ange katika doria zao hiuku wakitilkia mkazo ukaguzi wa kina wa wote ambao hushiriki uchukuzi wa nyama.

“Tumeimarisha njia zetu za kunasa ujasusi kuhusu sekta hii ya nyama. Tumefaniukiwa kunasa washukiwa 28 katika kipindi cha siku tat zilizopita na kufanikiwa pia kuvunja mltandao wa wizi huu wa mifugo katika Kaunti ya Nyandarua,” akasema.