• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Viongozi Lamu waahidi kuunga mkono ripoti ya BBI

Viongozi Lamu waahidi kuunga mkono ripoti ya BBI

Na KALUME KAZUNGU

VIONGOZI wa Lamu wamemwahidi Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwamba wataiunga mkono ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) na kuhakikisha imepitishwa bila kupingwa kwenye kaunti yao.

Viongozi hao, akiwemo Gavana Fahim Twaha, Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Ruweida Obbo na madiwani wa Bunge la Lamu wakiongozwa na Spika Abdul Kassim Ahmed wameahidi kuipigia debe BBI, wakisisitiza kuwa iko na manufaa tele kwa Lamu na nchi nzima kwa jumla.

Bw Twaha alitaja kipengele cha ripoti ya BBI sambamba na mswada uliopendekezwa wa nyongeza ya mgao wa fedha zinazoelekezwa kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi asilimia 35 kuwa muhimu kwa maendeleo nchini.

Alisema haoni sababu ya wananchi kupinga BBI ambayo azma yake ni kuafikia maendeleo mashinani.

“Ninawasihi watu wetu hapa Lamu wawe kitu kimoja na kuunga mkono ripoti ya BBI. Ikiwa fedha zinazotoka serikali kuu kuelekezwa kwa kaunti zitaongezwa, hiyo inamaanisha itakuwa rahisi kwa maendeleo kuafikiwa mashinani,” akasema Bw Twaha.

Mbunge Stanley Muthama alisema lengo la Rais Kenyatta ni kuleta umoja nchini.

“Hii ndiyo sababu akamleta kiongozi wa upinzani, Raila Odinga ili wafanye kazi pamoja kupitia handisheki. Pia yuko kwenye harakati za kuwaleta Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi. Tunahitaji Kenya moja kama Wakenya na tuepuke migawanyiko. Hii ndiyo sababu ninasisitiza kwamba tusielekezwe kwingineko. Tuunge mkono BBI hapa Lamu,” akasema Bw Muthama.

Kwa upande wake, Bi Ruweida Obbo aliwataka Rais na Bw Odinga kuondoa hofu kwani anahesabu kwamba tayari ripoti ya BBI imepitishwa Lamu.

Naye Spika wa Bunge la Lamu, Abdul Kassim Ahmed, alisema bunge liko tayari kuendeleza mchakato wa kupigia debe ripoti ya BBI kote Lamu ili ipite bila kupingwa eneo hilo.

Alisema BBI ni jawabu tosha kwa dhuluma za kihistoria za ardhi ambazo zimeshuhudiwa Lamu kwa miaka mingi.

Aliwataka wakazi wa Lamu kuja pamoja na kuunga mkono BBI kwa manufaa yao.

“Vile tuliungana mkono na kuangusha mswada wa Punguza Mzigo Bungeni ndivyo vile vile tutaungana kupitisha ripoti ya BBI. Ni ya manufaa tele kwa wananchi,” akasema Bw Ahmed.

Tangu ugatuzi ulipoanza kutekelezwa mwaka 2013 Lamu imekuwa ikipokea mgao wa chini zaidi wa fedha kutoka kwa serikali kuu ikilinganishwa na kaunti zote 47 za hapa nchini.

Pendekezo la kuongezwa kwa fedha za kaunti kutoka asilimia 15 ya sasa hadi asilimia 35 huenda likawa kichocheo kikubwa kwa wakazi wa Lamu katika kupitisha ripoti ya BBI.

Hii ni kwa sababu mara nyingi viongozi na wakazi wa Lamu wamekuwa wakiililia serikali kuu kuongeza mgao wa fedha eneo hilo ili kuwezesha maendeleo kuafikiwa.

“BBI ni suluhu ya kipekee kuona kwamba mgao wa fedha kutoka serikali kuu unaongezwa eneo letu. Hatuna sababu ya kutounga mkono BBI hapa Lamu. Ninaamini tutaipitisha kwa kauli moja,” akasema Bw Said Alwy.

 

 

  • Tags

You can share this post!

COVID-19: Visa vipya ni 724 huku watu 14 wakifariki

Ronaldo arejea ugani kwa matao ya juu baada ya kupona...