Habari Mseto

Viongozi Turkana waonya serikali kuhusu mapato ya mafuta

May 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY LUTTA

VIONGOZI wa kisiasa kutoka kaunti ya Turkana wamekubaliana kuwa hawataruhusu usafirishaji wa mafuta kutoka eneo hilo hadi serikali itawahakikishie kuwa jamii hiyo itapewa asilimia 10 ya mapato kutokana na mauzo ya rasilmali hiyo.

Viongozi hao kutoka mirengo ya NASA na Jubilee pia walisema sharti serikali iahidi kuipa serikali ya kaunti hiyo asilimia 20 ya mapato hayo.

Viongozi hao wakiwemo Gavana Josphat Nanok, Naibu Gavana Peter Lotethiro, Seneta Malachu Ekal, Mbunge wa Turkana Kusini James Lomenen, Mohammed Ali Lokuru (Mbunge wa Turkana Mashariki) na madiwani 11 waliahidi kuungana hadi pale “Turkana itakapopata mgao wake wa mapato kutokana na mauzo ya mafuta kufidia miaka mingi ambayo kaunti hiyo imetengwa kimaendeleo”.

Wakiongea Jumatatu mjini Lokichar, viongozi hao waliishutumu serikali kwa kusimamishwa kwa muda mwa Mswada wa Petroli wakisema hatua hiyo ilikuwa yenye nia mbaya.

“Tunamkashifu Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale kwa hatua hii ambayo ililenga kutunyima haki yetu ya kupata mgao wa mapato kutoka kwa rasilimali hii ambayo iko hapa kwetu,” akasema Gavana Nanok.

Bw Duale alisema alichukua hatua hiyo kutokana na kile alichotaja kama hatua iliyochangiwa na zaidi ya mabadiliko 50 yaliyofanyiwa mswada huo na Kamati ya Bunge kuhusu Kawi haswa baada ya kujumuishwa kwa maoni ya umma.

Mabw Lomenen na Lokiru ambao ni wanachama wa Kamati hiyo ya Kawi walimwomba Bw Duale kukubali marekebisho hayo hasa baada ya Naibu Rais William Ruto kuunga mkono pendekezo la kutengewa jamii ya Waturkana asilimia 10 ya mapato ya mafuta.

“Vile vile, Naibu Rais Bw William Ruto aliunga mkono pendekezo kwamba serikali ya kaunti itengewe asilimia 20 ya mapato, kando na asilimia 10 kwa jamii.

Duale anafaa kuheshimu ahadi hiyo ya Naibu Rais aliyotoa alipohudhuria Hafla ya Utamaduni wa Waturkana katika mjini Lodwar mnamo Aprili 20. Tupewe haki yetu la sivyo hatutaruhusu usafirishaji mafuta,” akasema Bw Lomenen.

Mbunge pia alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuunga mkono wazo hilo litakalopelekea eneo la Turkana kufaidi kimaendeleo.

“Ikiwa Rais angetaka kuacha kumbukumbu nzuri, basi hana budi kukubali kwamba jamii ya Waturkana watengewe asilimia 10 ya mapato ya mauzo ya mafuta,” akasema.