Viongozi wa dini North Rift wataka baadhi ya shule zisifunguliwe
NA TITUS OMINDE
VIONGOZI wa kidini kutoka North Rift wanataka serikali kukubali shule ambazo ziliathiriwa pakubwa na mafuriko kujiandaa vilivyo kabla ya kufunguliwa ili kutoa nafasi kwa ukarabati wa shule husika.
Askofu Zablon Malema wa Kanisa la Haleluya mjini Eldoret alisema kuna wazazi ambao bado wana wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wao shuleni ambao waliathiriwa pakubwa na mafuriko hivyo basi serikali inafaa kuzingatia wazazi kama hao ili kushughulikia hofu zao.
“Tunamshukuru Rais William Ruto kwa hatua yake ya kijasiri ya kutangaza kufunguliwa tena kwa shule lakini tunaiomba serikali pia kuzingatia wasiwasi wa wazazi katika maeneo ambayo shule ziliathiriwa vibaya na mafuriko ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi mbali na kutoa nafasi ya kukarabati miundo mbinu iliyobomolewa na mafuriko,” alisema Askofu Malema.
Askofu Malema hata hivyo amewahakikishia wazazi katika maeneo ambayo shule hazikuathiriwa vibaya kutohofia usalama wa watoto wao.
Alisema jinsi Mungu alivyosaidia Wakenya kushinda athari za Covid-19 Mungu huyohuyo ataisaidia nchi kukabiliana na athari za mafuriko.
“Watahiniwa wa KCPE 2020 ambao waliathiriwa na Covid-19 pia wameathiriwa wakati wa Kidato cha Nne kama watahiniwa wa KCSE, maombi yetu ni kwamba kila la kheri kwa wanafunzi hawa wote jinsi Mungu alivyotusaidia wakati wa janga la COVID-19 tutashinda mafuriko pia,” Askofu Malema alisema.
Hata hivyo, amewataka maafisa wote wa serikali katika maeneo mbalimbali nchini kuwa waangalifu zaidi wanafunzi wanaporejea shuleni na kuishauri serikali ipasavyo.
“Tunataka kuamini kuwa serikali itaweka mikakati yote kuhakikisha watoto wetu wanakuwa salama shuleni,” aliongeza askofu Malema.
Kwa upande wake Sheikh Abubakar Bini, mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya alitoa changamoto kwa serikali kuhakikisha kuwa maeneo ambayo yameathiriwa pakubwa na mafuriko yanapewa kipaumbele maalum kwa usalama wa wanafunzi.
Sheikh Bini aliwataka wahisani kuwasaidia wazazi na shule zilizokumbwa na mafuriko pakubwa kukarabati miundo mbinu.
“Sote tunapaswa kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha wanafunzi wanafungua tena shule lakini muhimu zaidi hatupaswi kuhatarisha maisha ya wanafunzi katika maeneo ambayo bado yanakumbwa na mafuriko kama vile Budalangi katika Kaunti ya Busia, Kaunti ya Tana River miongoni mwa maeneo mengine,” alisema Sheikh Bini.