Viongozi wa dini pia waliionja fimbo ya Nyayo
Na CHARLES WASONGA NA JUSTUS OCHIENG
Rais Mstaafu Daniel arap Moi ambaye alifariki Jumanne alikabiliana vikali na viongozi wa makanisa waliokosa utawala wake hasa kuhusu ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Wakati wa kupigania demokrasia ya vyama vingi mivutano ilishuhudiwa kati ya viongozi wa makanisa na serikali yake.
Wahubiri kama Alexander Muge, Henry Okullu, David Gitari, Ndingi Mwana a’Nzeki, Zacchaeus Okoth na Timothy Njoya waliongoza mchakato wa kupigania demokrasia, kati ya 1986 na 1992 na kumkasirisha rais Moi walionja makali ya serikali ya Moi.
Wakati huo, kanisa lilichukua jukumu la kuwakilisha kila sehemu ya maisha ya waumini, hata kisiasa kando tu na jukumu lake la kimsingi ya kuwalea kiroho.
Viongozi hao watakumbukwa kwa kukabiliana vikali na maafisa wa serikali ya Moi walipopinga utawala mbaya na kutetea mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa.
Baadhi yao kama Askofu Muge walikufa wakipiga ufisadi na ukadamizaji wa haki vita.Kasisi huyu mstaafu wa Kanisa la PCEA Timothy Njoya anafahamika kutokana na mchango wake katika kupigania kurejelewa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini mapema miaka ya 1990s.
Mnamo Julai mwaka wa 1990, Njoya aliungana na viongozi wengine wa kisiasa kushiriki maandamano ya kutetea kuondolewa kwa sehemu ya 2A ya katiba ya zamani ili kuruhusu kuundwa kwa vyama vingine vya kisiasa vishindane na KANU.
Katika maandamano hayo maarufu kama Saba Saba, polisi waliwakabili kwa nguvu kupita kiasi ambapo wengi waliuawa.
Wakati mmoja Kasisi Nyoya alicharazwa kinyama nje ya majengo ya bunge, Nairobi na wahuni waliodai kufadhiliwa na wanasiasa walioaminika kuwa watetezi wa utawala wa Mzee Moi.
Askofu Okullu alishambuliwa vikali ya viongozi wa Kanu katika miaka ya 1990s huku wengine wakishinikiza kukamatwa kwake kwa kuikosoa serikali ya Rais Daniel Moi kila mara.
Okullu ambaye alikuwa Askofu wa Dayosisi ya Maseno Kusini ya Kanisa la Kianglikana pia alishirikiana na viongozi wanaharakati wengine wa mageuzi kupigania mfumo wa utawala wa vyama vingi katika miaka ya 1990s.M
arehemu Okullu pia aliikosa serikali ya Moi kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni Dkt Robert Ouko.
Askofu Ndingi alijitokeza kama mtetezi jasiri wa masilahi ya wahanga wa mapigano ya kikabila katika eneo la Rift Valley katika mapema miaka ya 1990s.
Wakati huo Askofu huyu mstaafu alikuwa akihudumu kama Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nakuru.Hasa, alielekeza shutuma zake kwa utawala wa mkoa kwa kuchochea mapigano hayo kwa faida ya tabaka la wanasiasa wakuu katika utawala wa Kanu wakati huo.
Hii ndio sababu Askofu Ndingi hakuelewana na Rais Daniel Moi. ikizingatiwa kuwa maafisa wa utawala wa mkoa kiungo muhimu zaidi katika utawala wake na ndipo aliwapa mamlaka makubwa.
Jina la marehemu Gitari liligongwa vichwa vya habari kwa mara ya kwanza mnamo 1988 alipojitokeza hadharani kukosoa mfumo wa uchaguzi wa mlolongo.
Alikuwa pamoja Maskofu wenzaje Alexander Muge, Henry Okullu na Timothy Njoya chini ya mwavuli wa Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK).