Viongozi wa Jubilee wazomewa walipojaribu kufikisha ‘salamu’ za Uhuru
NA WANDERI KAMAU
VIONGOZI kadhaa wa Chama cha Jubilee (JP), Jumapili usiku walizomewa vikali na wakazi wa eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, walipojaribu kuilaumu serikali ya Kenya Kwanza kutokana na changamoto zinazoikumba nchi.
Wakiongozwa na mwanablogu Pauline Njoroge, viongozi hao walikuwa wamefika katika kanisa la Jesus Christ Compassion Ministries (JCM) katika eneo la By-Pass, “kuwafikishia wenyeji salama za Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta”.
Viongozi wengine waliwa ni wabunge wa zamani Jude Jomo (Kiambu) na Peter Mwathi (Limuru).
Hata hivyo, walipopewa nafasi na kiongozi wa kanisa hilo, mcheshi Muthee Kiengei, kuwahutubia wenyeji, viongozi hao walianza kuishambulia serikali kuhusu vile gharama ya maisha ilivyo juu, na jinsi imeshindwa kuwasaidia Wakenya kuepuka changamoto zinazowakumba.
“Kusema kweli, tulijichanganya mahali. Gharama ya maisha iko juu. Biashara za watu wetu katika eneo la Mlima Kenya zimefungwa. Wakenya hata hawana fedha za kusherehekea sikukuu ya Mwaka Mpya au hata kuwalipia karo wanao kutokana na ugumu wa maisha,” akasema Bi Njoroge.
Bw Jomo ndiye alifuata, akitoa kauli kama hiyo.
“Lazima tuseme yametosha! Mtaungana nasi kwenye vita vya kuwakomboa watu wetu?” akaulizwa Jomo.
Hata hivyo, wenyeji walianza kuwazomea viongozi hao, baadhi yao wakisema kwamba huo haukuwa wakati wa siasa.
Wengine walisikika wakiitetea serikali.
“Achana na serikali yetu!” wakasema baadhi ya watu kwenye umati.
Kelele zilipozidi, ilimlazimu mfawidhi kukatiza hotuba ya Bw Jomo, ambapo baadaye waliombewa na kuondoka.
Mcheshi Kiengei aliwakosoa watu waliowazomea wanasiasa hao, akisema kuwa kiongozi yeyote anafaa kupewa nafasi kujieleza.
Wadadisi walitaja tukio hilo kama ishara kwambatofauti za kisiasa zilizoibuka baina ya Bw Kenyatta na Rais William Ruto kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022 bado zipo.