Viongozi wa Kiambu washauriwa kushirikiana
Na LAWRENCE ONGARO
VIONGOZI kutoka Kaunti ya Kiambu wameshauriwa wasitishe malumbano ya kisiasa na badala yake wamjali mwananchi wa kawaida.
Mwanasaikolojia Bi Gladys Chania alisema katika siku za hivi karibuni madiwani wamekuwa wakizozana na gavana wao Dkt James Nyoro, na ni vyema kukomesha malumbano hayo.
Akizungumza kwa njia ya simu mnamo Ijumaa, Bi Chania alisema kwa muda mrefu Kaunti ya Kiambu haijapata amani kwa sababu viongozi wametekwa nyara na siasa za ubabe.
“Binafsi nisingependa kusikia mjadala wa kung’oa gavana Nyoro kwa sababu tangu ashike usukani amekuwa akiweka afisi yake kuwa sawa lakini malumbano kutoka kwa madiwani yamezidi,” alisema Bi Chania na kuongeza mwananchi wa kawaida hana haja na malumbano bali anataka maendeleo.
Aliwataka viongozi wote wajue ni miaka michache tu iliyosalia kipindi hiki na kwa hivyo waache vitisho vya kila mara kwa sababu kulingana naye, gavana anastahili kupewa nafasi ya kuchapa kazi.
Alisema gavana huyo amesalia na miaka miwili tu kwenda kwa uchaguzi wa 2022, na kwa hivyo miradi ya maendeleo inastahili kukamilishwa kabla ya wakati huo.
Alisema tayari madiwani wapatao 36 kati ya 92 wametia saini zao kwa mpango wa kumng’oa gavana Nyoro mamlakani huku akitaja kitendo hicho kama cha kuwakosea wananchi wa Kiambu.
Baadhi ya madiwani wanadai ya kwamba gavana wao hajawajulisha jinsi fedha fulani za maendeleo zimekuwa zikitumika.
“Ningependa kuwashauri viongozi hao waketi chini na gavana wao na kutatua maswala hayo kiungwana badala ya kutumia njia ya vitisho,” alisema Bi Chania.
Alisema kuwa Kaunti ya Kiambu ina idadi ya watu 1.2 milioni, na kwa hivyo inahitaji kuangaziwa zaidi kuhusu maendeleo.
Aliwashauri viongozi hao wavumiliane hadi mwaka wa 2022 ili wamchague kiongozi mwingine wanayemtaka ikifika wakati huo.