Viongozi wa Kiislamu watoa mapendekezo yao ya kufunguliwa kwa misikiti
Na WINNIE ATIENO
VIONGOZI wa dini ya Kiislamu kutoka Kaunti ya Mombasa wameanza kutoa mapendekezo yao kwa serikali kuhusu kufunguliwa kwa misikiti.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa tawi la Pwani la Muungano wa Waislamu Nchini (Supkem) Sheikh Mudhar Khitamy viongozi hao wamependekeza wakati wa swala kila muumini atatakiwa kujitenga na mwenzake.
Sheikh Khitamy ambaye amekuwa akikutana na viongozi wa dini wa Kiislamu kutoka wilaya za Kisauni, Likoni na Changamwe kwa pamoja wamependekeza waumini wapimwe jotomwili kabla ya kuingia misikitini.
“Jambo hilo halibatilishi swala, lazima tuepuke usambazaji wa virusi vya corona. Lazima watu waoshe mikono kabla kuingia misikitini na mwishowe kila mtu atatakiwa abebe mswala wake. Tumethibitisha kwa serikali kwamba tuko tayari kufungua misikiti lakini kwa masharti iliyoweka. Twaambia wale hawataki masharti waende kwingineko,” amesema Sheikh Khitamy.
Kiongozi huyo wa dini amewasihi waumini wa Kiislamu kufuata taratibu za Wizara ya Afya ili kuepuka usambazaji wa virusi vya corona.
Sheikh Khitamy amesema misikiti itanyunyuziwa dawa kama hatua mojawapo ya kuepushia waumini hatari ya virusi vya corona.
“Hakuna masharti magumu; kama huna mswala wako, beba shuka au hata leso au kitu chochote cha kuweka juu ya zulia,” akahimiza Sheikh huyo.