Habari Mseto

Viongozi wa UDA wataka ugavi wa nyadhifa ufanyike kwa maelewano, si uchaguzi

June 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA OSCAR KAKAI

BAADHI ya viongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Pokot Magharibi wamependekeza kuwe na makubaliano kuhusu nyadhifa za uongozi baada ya Mahakama Kuu kusimamisha kwa muda uchaguzi wa mashinani kutokana na kile ambacho chama hicho kilisema ni hofu kutokana na ghasia.

Viongozi hao wanasema kuwa mpango wa kwanza ulikuwa wa makubaliano baada ya wao kukutana mjini Kitale ambapo walikubaliana lakini wenzao wakawageuka.

Haya yanajiri baada ya uchuguzi wa maeneobunge, ambao ulikuwa umeratibiwa kufanyika Mei, 31, 2024, kuahirishwa kutokana na kile ambacho chama kilisema ni hofu ya ghasia baada ya Mahakama Kuu ya Kapenguria kuahirisha uchaguzi kwenye maeneobunge matatu ya Kapenguria, Kacheliba na Pokot Kusini. Uchaguzi huo pia ulikosa kufanyika katika eneobunge la Sigor.

Baraza la kitaifa la chama cha UDA Jumamosi lilisimasisha kwa muda uchaguzi huo kwenye kaunti za Nairobi, Pokot Magharibi na Narok.

Viongozi hao akiongozwa na mbunge wa Kapenguria Dkt Samuel Moroto wanadai kuwa kulikuwa na utepetevu na makosa wakati wa kupiga kura kuanzisha kwenye ngazi ya wadi kwenye kaunti.

Viongozi hao wanasema kuwa watu kutoka mrengo wa upinzani walishiriki kwenye uchaguzi ambao uliharibika wa mashinani kwenye kaunti hiyo.

“Tunataka makubaliano kwa sababu ndio kitu tulkubaliana wakati tulikutana mjini Kitale. Hatungepigana na Gavana sababu anahitaji hashima. Tungempa seneta nafasi nyingine na hata mbunge wa Sigor kupewa nyingine,” alisema.

Dkt Moroto ambaye aliongea katika eneo la Riwo anasema kuwa watu kutoka upinzani wamejiunga kwenye chama hicho na kuleta mapinduzi ndani yake.

“Tunafaa kukubaliana sababu viongozi wengine wamekuwa wajanja na wamekuwa wakinunua wapiga kura,” akasema.