• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Viongozi waendelea kuzungumza kuhusu unga usio salama kwa ajili ya binadamu

Viongozi waendelea kuzungumza kuhusu unga usio salama kwa ajili ya binadamu

Na LAWRENCE ONGARO na SHABAN MAKOKHA

SERIKALI inastahili kuchukua hatua kali kwa wanaosaga mahindi na kuwauzia wateja unga mbovu hasa katika supamaketi na maduka mengine.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, amempongeza Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) Bw Benard Njiraini kwa kuchukua hatua ya kusitisha kuuzwa kwa unga uliotajwa kwamba ni hatari kwa afya ya binadamu.

Serikali ilisitisha baadhi ya unga kuendelea kuuzwa katika maduka ya jumla. Baadhi ya chapa za unga zilizotajwa si salama kwa afya ya binadamu ni, Dola, Kifaru, Starehe, 210, na Jembe.

Ni hatua ambayo Kebs ilisema imetokana na ripoti ya vipimo vinavyosema unaweza kusababisha maradhi ya kansa kutokana na chembechembe nyingi za aflatoxin.

“Ni aibu kuona ya kwamba wale watu wanaopewa jukumu la kukagua bidhaa bora kwenye masoko ndio wa kwanza kupeleka bidhaa mbovu katika maduka. Ni vyema watu kama hao wachukuliwe hatua ya kisheria mara moja,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo Jumatatu eneo la Landless mjini Thika alipokutana na waumini wa kanisa moja eneo hilo.

Alisema ni vyema serikali kulinda afya ya wananchi ili wasizidi kuugua maradhi ya kansa ambayo yamekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Kenya.

“Iwapo tungetaka kuokoa afya ya wananchi wetu, basi ni vyema kufanya mambo kwa njia inayostahili ili kila kitu kiendeshwe kwa uwazi bila njia ya mkato,” alisema Bw Wainaina.

Alisema ni aibu kubwa sana kupata ya kwamba unga unaotumika na binadamu ukiwa umewekwa madukani na waliofanya hivyo wanaelewa kweli ni hatari kwa afya ya binadamu.

“Wale wote wanaohusika na jinsi ya kuendesha mambo kwa uwazi, lakini waliregea kutekeleza wajibu wao wanafaa kuchukuliwa hatua mara moja kwa sababu hiyo ni njia moja ya kucheza na afya ya binadamu,” alisema mbunge huyo.

Bidhaa nyingine alizotaja kama ni hatari kwa usalama ni samli aina ya Peanut Butter.

Alisema bidhaa hiyo ikikosa kuhifadhiwa vyema huharibika na kuleta hatari ya aflatoxin.

Siku chache zilizopita viongozi kadha pia walitoa malalamiko yao kuhusu mahindi hatari inayouzwa katika maduka ya jumla huku ikiwa ni hatari kwa afya ya binadamu.

Viongozi mbalimbali wanataka hatua ya haraka ichukuliwa dhidi ya wanaohusika na kuzikubalia kupelekwa kwenye maduka kwa matumizi.

Na katika kaunti ya Kakamega, baadhi ya viongozi sasa wanataka maafisa wa Kebs wanaosema wameshindwa kulinda raia, wanafaa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kakamega katika Bunge la Kitaifa Elsie Muhanda alidai baadhi ya maafisa walikubalia wasagaji nafaka kuingiza sokoni unga hatari ikiwa ni baada ya utoaji na upokeaji hongo.

Septemba 2019 Kebs iliruhusu kampuni kadhaa za unga kuendelea kuuza unga.

Kampuni zilizoathirika ni Pan African Grain (Starehe), Alpha Grain Ltd (Kifaru), Kitui Flour Mills (Dola), Kenblest Ltd (210) and Kensalrise Ltd (Jembe).

Bi Muhanda anataka serikali kufuatilia suala hilo kuwapa wanunuzi bidhaa kiini cha unga hatari kupatikana madukani kabla ya Kebs kufuta leseni za kampuni hizo mnamo Jumamosi wiki jana.

“Maafisa wa Kebs wamepotosha na kuwaelekeza kusiko Wakenya watumiaji wa bidhaa hizi za nafaka kwa sababu ni wajibu wake kuhakikisha ubora wa bidhaa zinazoingia sokoni,” akasema Bi Muhanda akiwa katika msikiti wa Lufumbo akitoa mchango wa hema kwa wafanyakazi wa afya ya jamii wa kutoka Butere mnamo Jumatatu.

Wasagaji nafaka hata hivyo wanasema walinunua mahindo kutoka Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) wakati ikiuza magunia milioni mbili ya mahindi kwa umma.

Mkazi wa Mumias Bw Fadhil Eshikwekwe amelalamika kuhusu suala hilo la bidhaa hatari sokoni.

“Mwaka 2018 tuliletewa sukari hatari na sasa leo hii tunaambiwa kuhusu unga wenye sumu inayosababisha kansa. Hawa maafisa wa serikali wanaochangia chakula hatari kuingia sokoni wana nia gani kwa Wakenya,” akauliza Bw Eshikwekwe.

  • Tags

You can share this post!

Walia waliozua fujo wako huru

Hakuna mikopo ya muda mfupi kwa serikali za kaunti –...

adminleo