Vipi nitajibu mashtaka na sielewi Kiingereza? mwanafunzi amuuliza jaji
Na PHYLIS MUSASIA
KULITOKEA kioja Jumatano katika Mahakama Kuu ya Nakuru mshukiwa wa mauaji ambaye pia ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili, alipodai mbele ya jaji kuwa haelewi Kiingereza na kwa hivyo hangeweza kujibu mashtaka dhidi yake.
Frankline Ngetich, 18, anayesomea katika shule ya upili ya Tumaini eneo la Barut eneobunge la Nakuru Magharibi, alichekesha korti aliponena kwa ujasiri kuwa lugha ya Kiingereza kwake ni kizungumkuti kwa hivyo ingekuwa vigumu kumuelewa karani wa korti wakati wa kumsomea mashtaka yanayomkabili.
“Sielewi Kiingereza mimi. Ninaomba korti itumie lugha ya Kiswahili ili iwe rahisi kwangu kujibu,” alisema Ngetich kwa ujasiri.
Jaji Joel Ngugi, alitaka kujua kwa nini mshtakiwa hakuweza kuelewa lugha ya Kiingereza hata baada ya kueleza korti kuwa alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili.
“Umetwambia kwamba una miaka 18 na kwamba uko kidato cha pili. Kwa nini huelewi lugha ya Kiingereza? Kwani huko shuleni hamfunzwi lugha?” akauliza jaji Ngugi kwa mshangao.
Hata hivyo, kesi haikukomea hapo kwani mshtakiwa alipaswa kujibu mashtaka ya kumuua mwalimu wa shule jirani ya Hope Well, Bw Peter Omare Mogusu mnamo Januari 24, 2019.
Kulingana na maelezo ya mkurugenzi mkuu wa shule ya upili ya Hope Well Bw Vitalis Kahenda, mshukuiwa aliungana na wenzake wawili ambao hawakuwa mahakamani kutekeleza kitendo hicho kilichopelekea marehemu kupoteza uhai wake pindi tu alipofikishwa hospitalini kupokezwa matibabu..
Watatu hao wanasemekana kumvamia Bw Mogusu usiku wa Januari 24 mwendo was saa nne alipokuwa akirejere nyumbani kwake karibu na shule hiyo.
“Bw Mogusu amekuwa mwalimu wetu wa Fizikia na maswala ya kompyuta baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu cha Maseno mwaka wa 2016,” akaeleza Bw Kahenda.
Aliongeza kuwa, “washukiwa walimvamia na kumpiga kifaa butu kichwani jambo ambalo lilimsababishia majeraha mabaya yaliompelekea kukataa roho pindi tu alipofikishwa hospitalini.”
Mmoja wa washukiwa ambaye alikuwa mwanafunzi wake Bw Mogusu anasemekana kuapa kulipiza kisasia baada ya mwalimu huyo kuchukua simu aliyokuwa nayo shuleni kinyume na sheria.
Mshukiwa Ngetich hata hiyo, alikana mashtaka dhidi yake na kuomba kuachiliwa kwa dhamana.
Upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo ukidai kuwa usalama wa mshtakiwa uko katika hali ya hatari kulingana na joto liliko kwa wakazi wa eneo alikotoka Bw Mogusu.
Korti iliamuru kuwa azuiliwe korokoroni hadi jumatano wiki ijayo atakaporudishwa mahakamani kwa maelekezo zaidi.