Habari Mseto

Visa vya unyakuzi wa vipande vya ardhi vyazidi Thika

December 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

ARDHI ya umma iliyonyakuliwa katika eneo la Ngoingwa, Thika itarejeshwa chini ya umiliki utakikanao kulingana na barua iliyowasilishwa kwa afisi kuu ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC).

Wakazi wa Ngoingwa waliungana pamoja juzi na kuwasilisha malalamiko yao kwa mbunge wao Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina ambaye tayari amechukua hatua.

Mwanzo wa mwezi Disemba, mbunge huyo aliandika barua kwa tume ya ardhi akitaka wanyakuzi hao wa ardhi hiyo waregeshe kipande hicho kwa sababu ni mali ya umma.

Kulingana na barua hiyo, ni kwamba pahala paliponyakuliwa palikuwa pa kujengwa uwanja wa shule ya msingi na mahitaji mengine muhimu ya umma.

“Unyakuzi wa vipande vya ardhi umekuwa mwingi eneo hili na kwa hivyo sitakubali mtindo huo uendelee kwa sababu walaghai wamekuwa hatari kwa usalama wa wakazi,” alisema Bw Wainaina.

Alisema baada ya kuwasilisha barua hiyo kwa afisi kuu ya ardhi mjini Thika sasa itabidi vyeti vyote vya umiliki vilivyotolewa hapo awali vifutiliwe mbali.

Aliyasema hayo mnamo Ijumaa alipozuru eneo hilo ili kujionea mwenyewe na macho yake.

Kulingana na barua hiyo ilidaiwa watu wengi wamelaghaiwa mashamba yao huku wakiachwa katika hali ngumu kimaisha.

“Watu watakaopatikama na makosa ya kunyakua ardhi katika eneo ka Thika watalazimika kujitetea wenyewe,” alisema mbunge huyo.

Alisema tayari amewarai maafisa wa ardhi kutoka jijini Narobi waje mjini Thika mwezi Januari 2021 ili waendeshe kliniki ya kuwahamisha wananchi jinsi ya kununua ardhi na kupata vyeti halali.

Alisema tayari idara ya tume ya ardhi inagonjewa kwa hamu ili kuweka kliniki mjini Thika na kuwahamashi jinsi ya kuwa na ardhi na idara ya ardhi itafanya juhudi kuona ya kwamba maswala ya ardhi inajazwa kupitia mtandao ili kupunguza ulaghai.

Baadhi ya watu waliopitia mtego huo wa utapeli wa ardhi ni watu wakongwe.

Ilidaiwa watu wengi wamepoteza hamu ya kununua ardhi eneo la Ngoingwa kwa sababu wanaogopa kukosa cheti cha umiliki.

Bw Martin Karanja ambaye ni mkazi wa Ngoingwa alisema wakazi wengi wamepoteza ardhi zao kwa sababu ya kupokea cheti iliyokuwa imepata mnunuzi mwingine.

“Hatua kali ikichukuliwa na time ya ardhi (NLC) itafanya wengi waliozoea kupata ardhi kwa njia ya mkato wakose mweleke,” alisema Bw Karanja.

Siku chache zilizopita kiongozi mmoja wa eneo hilo alishambuliwa na watu baada ya kuwa mstari wa mbele kutetea wananchi kuhusu unyakuzi wa ardhi.