• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Visa vya watu kujaribu kujitoa uhai na wengine kujitia kitanzi vyaongezeka Mombasa

Visa vya watu kujaribu kujitoa uhai na wengine kujitia kitanzi vyaongezeka Mombasa

Na MISHI GONGO

MWANAMUME mmoja mjini Mombasa anaendelea kupokea matibabu baada ya kujaribu kujitoa uhai kwa kunywa sumu Jumapili.

Inadaiwa alikunywa sumu baada ya kuzozana na rafiki yake.

Akithibitisha tukio hilo Afisa mkuu wa polisi eneo la Changamwe Bw Khalif Abdullahi alisema kuwa mwanamume huyo kutoka mtaa wa mabanda wa Kibarani alipatikana na majirani akiwa katika hali mahututi na kupelekwa katika hospitali ya Port Ritz ambako anaendelea kupokea matibabu.

Kulingana na afisa huyo, visa vya watu kujaribu na hata kujitoa uhai vimeongezeka maradufu tangu kuzuka kwa janga la corona.

Alieleza kuwa visa 10 vimeripotiwa katika eneo hilo.

“Inasikitisha kuona watu wanaendelea kujitoa uhai, tunawashauri watu kutafuta usaidizi katimka wataalamu wa afya ili kukabili msongo wa mawazo. Tunataka watu watambue kuwa kujitoa uhai si suluhisho,”akasema.

Aidha aliongezea kuwa wengi wanaojitoa uhai huwa wanapitia matatizo ya kimaisha.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) mtu mmoja hujitoa uhai kila baada ya sekunde 40.

Shirika hilo lilitaja msongo wa mawazo kuchangia katika watu kujitoa uhai.

Lilisema kuwa watu wengi hujitoa uhai baada ya kukumbwa na matatizo na kushindwa kukabili msongo wa mawazo unaotokana na hali hiyo.

Shirika hilo lilitaja mafarakano ndani ya nyumba na baadhi ya watu dhaifu katika jamii kuwa sababu za matukio kama hayo.

Wengi wa wanaojitoa uhai huwa hawatambui kuwa wana tatizo na kukosa kutafuta msaada kwa muda unaofaa.

Wengi hutambua wakati hali yao imefika mwisho.

Visa vya kusikitisha zaidi vya watu kujitoa uhai Mombasa ni vile vya msichana aliyekuwa na umri wa miaka 14 kujitoa uhai baada ya kuagizwa arudie darasa la nyuma, mwalimu kujitoa uhai eneo la Changamwe baada ya ya kupoteza ajira kufuatia kuzuka kwa janga la corona na kuachwa na mkewe na kisa cha mwanamume kumnyonga mkewa eneo la Mishomoroni.

You can share this post!

Hakuna kupumua shuleni

VIFO: Joho awahimiza wakazi wa Mombasa wazingatie kanuni za...