Habari Mseto

Visa vya wizi wa tuktuk vyaongezeka Githurai

September 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

KWA zaidi ya miaka mitatu shughuli za usafiri na uchukuzi mitaani Githurai 44, Nairobi na Githurai 45 zimerahisishwa na magari madogo aina ya tuktuk.

Nauli ya vijigari hivyo ni nafuu ikilinganishwa na bodaboda.

Hata hivyo, wahudumu wake sasa wanalalamikia kuongezeka kwa visa vya wizi wa vijigari hivyo.

Chini ya muda wa miezi miwili pekee, tuktuk tatu zimeripotiwa kuibwa.

“Ni jambo la kusikitisha kuona uwekezaji wetu ukianza kuhangaishwa na wahuni. Kisa cha hivi punde ni cha mnamo Jumatatu wiki hii, ambapo tuktuk iliyonunuliwa mwaka huu imeibwa,” naibu mwenyekiti wa muungano wa Githurai Tuktuk Association (GTA) Laban Gitonga ameambia Taifa Leo.

Mtaa wa Githurai 45, ambao vijigari vyake huhudumu kati ya Progressive, Mumbi, Mwihoko na St Augustine, una zaidi ya tuktuk 300. Aidha, tuktuk mpya hugharimu zaidi ya Sh415, 000.

Kulingana na Bw Gitonga, wahuni wanaotekeleza wizi huo wanalenga tuktuk mpya.

“Tuktuk zilizoibwa, mbili ni mpya na moja imehudumu miaka kadhaa,” akasema.

Mwaka 2017 tuktuk yenye nambari za usajili KTWB 108A ilikuwa imeripotiwa kuibwa na siku mbili baadaye ikapatikana operesheni kali miongoni mwa wahudumu ilipoendeshwa.

Pia, visa vya wizi wa pikipiki Kiambu na Nairobi si vigeni.

Ni muhimu kutahadharisha kwamba wizi wa magari unahusishwa na visa mbalimbali vya uhalifu, ambapo gari linaweza kutumika kusafirisha dawa za kulevya na mihadarati au kufanya mauaji. Katika hali hiyo, mmiliki atajipata kuandamwa na mkono wa sheria.

“Gari lolote lile linapoibwa, hatua ya kwanza iwe kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu ili shughuli za kulitafuta lianze. Pia, hatua hiyo itamlinda mmiliki dhidi ya maovu yanayoweza kutekelezwa nalo,” ashauri Charles Mwangi, afisa wa polisi jijini Nairobi.

Teknolojia inaendelea kuimarika, na wamiliki wa magari wanahimizwa kuyatia vifaa fiche, traka, kuyafuatilia. Bw Laban Gitonga amesema GTA inapania kushawishi wamiliki kukumbatia mfumo huo.