Habari Mseto

Vita vya kijamii Narok, Kisii vyasambaratisha maisha vijana wakipigana kwa mishale

Na RUTH MBULA March 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VITA vya kikabila ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa katika kaunti za Kisii na Narok vimesambaratisha maisha, wengi wakilazimika kuhama makwao na njia zao za kupata riziki kulemazwa.

Wikendi, vijana kutoka eneo la Mapishi Trans Mara na wenzao kutoka Nyagenke, Kaunti ya Kisii walikabiliana kwa zaidi ya saa tano.

Vita hivyo, vilionekana kulemea hata polisi ambao walifyatua risasi hewani na kuwarushia vijana hao gesi za kutoa machozi.

“Vijana hao walianza kuzua taharuki baadaye mnamo Jumamosi mchana lakini maafisa wetu wapo hapa kuhakikisha kuna usalama,” akasema Naibu Kamishina wa Kenyenye William Bett mnamo Jumamosi.

Katika vita hivyo, vijana hao wamekuwa wakitumia mishale, rungu, panga na silaha nyingine butu huku mtu mmoja akiaga dunia.

Wengine 10 nao wamekuwa wakitibiwa majeraha ya mishale kwenye hospitali za Kisii na Narok.

Kuzuka kwa mapigano hayo hasa kumewaathiri wanawake, watoto ambao sasa wamelazimika kutorokea usalama wao. Wengi wa waliohepa sasa wanaishi kwenye nyumba za wasamaria wema.

“Vita hivi vinashangaza kwa sababu hatupiganii chochote. Wizi wa ngómbe ulitokea mbali sana kwetu ambapo sasa vita vimechacha,” akasema Mzee James Mogaka.

Kati ya maeneo ambayo bado kuna taharuki ni Nyagenke, Nyabitunwa, Kiango, Mapashi na Shankoe.

Utata ulianza pale ambapo ngómbe watatu waliibwa upande wa Kisii na kutoweka upande wa Narok wiki jana.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii Kisii Dkt Douglas Mariita alithibitisha kuwa walikuwa wamepokea vijana wenye majeraha ya mishale.

“Mmoja alikuwa na mshale shingoni na iliwachukua madaktari wetu muda wa saa sita kuondoa mshale huo,” akasema Dkt Mariita.

Mbunge wa Kilgoris Julius Sunkuli na mwenzake wa Bomachoge Borabu Obadiah Barongo, wote waliandaa mkutano Jumamosi iliyopita na wakawaambia wafuasi wao wasalie tulivu.

“Wazee kutoka Trans Mara wamekubali kufuatilia suala hilo na kuhakikisha ngómbe walioibwa wanarejeshwa. Nawaomba msalie watulivu,” akasema Bw Barongo.

Bw Sunkuli naye alisema jamii za mpakani zimeishi kwa amani na vijana hawafai kuzua machafuko.

“Si vyema kuvaamiana kuhusu masuala ambayo yanaweza kusuluhishwa kupitia mazungumzo,” akasema.

Wazee kutoka jamii hizo mbili waliwaomba vijana wasitishe mapigano na wakaahidi kuwa ngómbe walioibwa watasakwa na kurejeshwa.

Mkutano wa usalama ulioandaliwa Kilgoris uliafikiana kuwa iwapo ngómbe hao waliibwa, basi wanastahili kufuatiliwa na machifu kutoka jamii hizo mbili kwa ushirikiano.

Naibu Kamishina wa Trans Mara Jack Musua alisema wezi hao wanastahili kushughulikiwa kibinafsi badala ya jamii yote kulaumiwa.

Visa vya ghasia si mapya eneo hilo. Mnamo 2023, mvulana mwenye umri wa miaka 15 aliaga dunia na nyumba 20 na ekari 50 za miwa kuteketezwa huku wengi wakiumia.

Mnamo 2020, watu wawili walijeruhiwa vibaya kwenye Lokesheni ya Olememil. Nayo mnamo 2015, mwanaume aliuawa na nyumba kadhaa kuteketezwa wakati ambapo mkutano wa usalama ulikuwa ukiendelea eneo ambalo si mbali na pa mahala pa mapigano.