• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Vituko na vurumai katika mazishi ya Brian Chira

Vituko na vurumai katika mazishi ya Brian Chira

NA ELIZABETH NGIGI

MWIGIZAJI wa TikTok Brian Chira alizikwa Jumanne katika kjiji cha Gitei, Gathanje, Kaunti ya Kiambu katika mazishi yaliyojaa vituko.

Mazishi yake yalivutia umati mkubwa wa watu mashuhuri katika kundi lake la kuunda maudhui ya burudani linalofahamika kama ‘Chira Clan,’ na kuacha wanakijiji kwa mshangao.

Wanakiijiji hawakuwa wameona umati mkubwa wa vijana kama huo ambao ilikuwa vigumu kuuthibiti.

Marafiki na mashabiki wa Chira hawakuheshimu hata wazee katika kijiji hicho.

Kwa kawaida, Brian, 23 angezikwa na jamaa zake wa karibu, waliosoma naye na baadhi ya majirani.

Hata hivyo, haikuwa hivyo kwa kuwa hata viongozi wa kidini hawakupatiwa fursa ya kuongoza ibada kando ya kaburi.

Vurumai zilizuka huku mamia ya watoaji burudani katika TikTok wakikusanyika na kuzingira kaburi, baadhi yao wakiwa walevi na kutojali kamwe.

Wanakijiji na hata watu wa familia walitazama kwa mshangao na kuwaruhusu kumzika rafiki yao bila kuelewa walichokuwa wakifanya.

Badala ya kufunika kaburi kwa mchanga, waliutawanya na kuanza kupanda maua. Walisakata densi, wakarekodi video na kujipiga selfie katika kaburi la Chira.

Baada ya mazishi, walifanya matambiko katika kaburi la Chira, ikiwemo kutumia pombe kunyunyuzia maua waliyopanda.

Taifa Leo ilizungumza na baadhi ya majirani ambao walikasirishwa na matukio katika mazishi hayo.

Mwanakijiji mmoja alihuzunishwa na maneno waliotumia wanaTiktok hao kama ‘Hatuna maisha’.

“Tunawatakia mema tu watoto wetu kwa sababu hatungetaka kushuhudia tulichoona leo (Jumanne). Ilikuwa hali mbaya sana. Hata familia haikuruhusiwa kuzika mpendwa wao kwa heshima. Tunataka watoto wetu kurudi nyumbani kwa heshima ambayo waliondoka wakiwa nayo,” alisema mwanakijiji huyo.

Matumaini yao ni kwamba hawatashuhudia tabia kama hiyo tena katika kijiji chao.

“Tunaomba kijiji chetu kuandaa tambiko la kukitakasa kuondoa mapepo mabaya yaliyoachwa na vijana hao,” akasema.

Ni nini hasa kiliwakasirisha zaidi?

“Hatukutaka jinsi walivyokuwa wamevalia, kuvuta sigara na kulewa pombe mbele yetu. Hawakuwa na heshima hata kwa viongozi wa kidini. Walipuuza mila zetu za Kikuyu na hatukuwa tumewahi kuona tabia kama hiyo. Walikuwa wakikojoa kila mahali. Hatukulelewa hivyo. Tunasikitikia maisha yao ya baadaye na watakavyolea watoto wao,” alieleza mzee mmoja.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa kidini Laikipia walalamikia ujangili, kuzorota...

Tshisekedi na Kagame wakubali kukutana kujadili amani...

T L