Habari Mseto

Vizingiti vyaongezeka katika juhudi za kumshtaki wakili

June 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

HAIJULIKANI ni lini wakili Assa Nyakundi atajibu shtaka la kumuua mwanawe baada ya mahakama kuu kuweka breki kushtakiwa kwake kufuatia ombi la kuhoji uhalali wa shtaka hilo.

Kesi hiyo iliahirishwa Ijumaa na Jaji James Wakiaga kuwawezesha mawakili Dkt John Khaminwa, Haroun Ndubi na wakili wa familia Dunstan Omari kuwasilisha maombi ya kuhoji uhalali wa shtaka la mauaji alilowasilisha Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).

“Kesi hii inakumbwa na kizugumkuti kwa vile DPP amemfungulia wakili Nyakundi mashtaka mawili kutokana na tukio moja,” walisema mawakili Khaminwa na Ndubi.

Mahakama ilifahamishwa kuwa kuna kesi ya kuua bila ya kukusudia dhidi ya Bw Nyakundi iliyowasilishwa katika mahakama ya Kiambu.

Hata kabla ya kesi hiyo kuamuliwa, DPP aliwasilisha ombi la kuitamatisha na ombi hilo halijasikizwa katika mahakama ya Kiambu.

Pia, kuna ombi lingine ambapo hakimu anayeisikiza ameombwa ajiondoe na DPP.

Huku haya yakijiri, DPP aliwasilisha shtaka lingine la mauaji dhidi ya Nyakundi.

Mawakili Dkt Khaminwa na Ndubi walimweleza Jaji Wakiaga kuwa watawasilisha maombi mawili ya kufutiliwa mbali kwa kesi hiyo ya pili.