Vurugu makazi yakibomolewa Mukuru
NA SAMMY KIMATU
MAAFISA wa polisi Kupamabana na Ghasia (GSU) Jumatano, Juni 12, 2024 walilazimika kufyatua mikebe ya vitoza machozi ili kukabiliana na kundi la vijana waliokuwa wakitupa mawe kuvuruga shughuli za kubomoa nyumba eneo la Mukuru, Nairobi.
Kwa takriban saa moja ya makabiliano, shughuli zilisimama katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Maasai, tarafa ya South B, Kaunti Ndogo ya Starehe.
Akiongea na Taifa Leo Dijitali, mkuu wa Kaunti Ndogo ya Starehe, John Kisang alisema hali ilitulia baada ya polisi kufanikiwa kutimua vijana hao.
Ripoti zilieleza kwamba nia ya vijana hao ilikuwa kupora mali ya watu katika nyumba zilizobomolewa sawa na ambazo wapangaji walikuwa wamefunga kwa kufuli na kuenda wanakofanya kazi.
“Vijana hao ni wahuni. Nia yao ilikuwa kuiba na kuvunja nyumba za wakazi ambao walikuwa kazini hata licha ya kuwa hazijalengwa kubomolewa,” Bw John Kivuitu, mkazi, akasema.
Bw Kisang alisema tingatinga lilikuwa likiendelea kubomoa nyumba na vibanda katika eneo la mkondo wa maji katika mto Ngong.
“Serikali ilikuwa ikiondoa majengo na vibanda katika maeneo yaliyopimwa na kupatikana yamo ndani ya mkondo wa maji mkabala mwa mto Ngong,” Bw Kisang akasema.
Kadhalika, afisa huyo alisisitiza kwamba serikali inafuata utaratibu wakati wa zoezi la kuondoa wakazi huku ikimakinika kuwaondoa kiutu.
Alisema katika mchakato huo, kwanza, wapangaji na wamiliki wa nyumba au vibanda wanaarifiwa na kisha kuonyeshwa alama iliyowekwa kuashiria umbali rasmi wa kuwa mita 30 kutoka kwa mto.
Kisha, wanapewa muda wa kuondoa au kubomoa mabati na kubeba mali yao, kabla ya matingatinga kuanza shughuli za ubomoaji.
Bw Kisang alihoji kwamba zoezi hilo linaendeshwa kwa mujibu wa agizo la Rais Dkt William Ruto la kubomoa nyumba zilizoko karibu na mto Ngong, Mto Mathare na mto Nairobi.
Hata hivyo, wakaazi katika mitaa ya mabanda maeneo ya Mukuru hasa eneo la Starehe, Makadara na Embakasi Kusini walisema wanahangaika kwa kukosa nyumba za kukodi kwa sababu watu ni wengi na nyumba za kuwahifadhi zimeadimika.
Hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii, wakazi hao walidai hawakuwa wamepokea kitita cha Sh10,000 walizoahidiwa na serikali ili kuwawezesha kugharamia ada ya kuhamisha mali yao.