Wa Iria akana shtaka la ufisadi wa Sh351m
NA RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria ameshtakiwa kuhusu ufisadi wa Sh351 milioni, shtaka ambalo amekanusha.
Bw Wa Iria ameshtakiwa kwa njama ya kulaghai umma Sh351 milioni kwa njia ya ufisadi.
Alishtakiwa pamoja na David Maina Njeri, na Solomon Mutura Kimani ambao walikuwa wakurugenzi wa kampuni ya matangazo kwa vyombo vya habari ambayo ilidaiwa kujipatia Sh351,097,491.15 kinyume cha utaratibu wa kisheria, wakidai kuwa kampuni hiyo ya habari ilitoa huduma kwa kaunti.
Naye Bw Njeri wa Top Image Media Consultant Limited, anadaiwa kutekeleza uhalifu kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba 21, 2014, na Juni 19, 2017.
Bw Wa Iria alikabiliwa na mashtaka ya mgongano wa maslahi na utakatishaji wa fedha. Alishtakiwa kwa kujinufaisha moja kwa moja kupitia kandarasi kati ya Top Image Media Consultant Limited na Serikali ya Kaunti ya Murang’a.
Hakimu mkuu wa mahakama ya kukabiliana na ufisadi Thomas Nzioki, alifahamishwa kwamba gavana huyo wa zamani alipokea Sh31,829,800 kutoka kwa Top Image Media kinyume cha sheria.
Kuhusu utakatishaji fedha, inadaiwa Bw Wa Iria pamoja na wakurugenzi wa Top Image Media, waliingia katika mpango wa uhamisho wa Sh7.5 milioni kwa ununuzi wa kipande cha ardhi nambari Nairobi/Block 83/14/309 katika eneo la Umoja Innercore.
Watatu hao pia wanakabiliwa na shtaka jingine la utakatishaji fedha kuelekea ununuzi wa nyumba mbili–Batian 4 na Nellion 88–zilizoko katika eneo la Mlima Kenya.
Soma Pia: Kiini cha masaibu ya Wa Iria
Upande wa mashtaka unadai kuwa pesa hizo zililipwa kutoka kwa Serikali ya Kaunti ya Murang’a hadi Top Image Media kama njia ya kuficha chanzo cha pesa hizo.
Gavana huyo wa zamani alishtakiwa kwa kujipatia Sh600,000 za kuchimba kisima kutokana na pesa zilizolipwa kinyume cha utaratibu na serikali ya kaunti mnamo Desemba 2015.
Mahakama ilifahamishwa kwamba Bw Wa Iria ambaye pia alikuwa mkurugenzi wa Top Image Media na Value View Limited, alihamisha Sh3 milioni kinyume cha utaratibu.
Gavana huyo wa zamani pia alishtakiwa kwa kutumia Sh3.7 milioni pesa za kaunti, kununua ekari 13 za ardhi huko Mueiga.
Lakini Bw Wa Iria alikanusha mashtaka hayo, akidai kwamba anawindwa kisiasa.
“Sina hatia, similiki kipande hicho cha ardhi na ninalengwa kisiasa,” alisema Bw Wa Iria.
Akiomba kuachiliwa kwa mteja wake kwa bondi, Kigogo wa Wiper Kalonzo Musyoka aliitaka mahakama kuzingatia kanuni ya uaminifu kwa Katiba.
Pia alimtaka Bw Nzioki kuchukua tahadhari ya mahakama kwamba Bw Wa Iria sio tu gavana wa zamani wa Murang’a, bali pia kiongozi wa chama cha kisiasa cha Usawa, ambacho ni kimojawapo cha vyama wanachama katika muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya.
“Kulengwa kwa mwanachama wa muungano, ama awe ni wa Kenya Kwanza au Azimio, kunaingilia kanuni za demokrasia ya vyama vingi,” akasema Bw Musyoka.
Kiongozi huyo wa Chama cha Wiper alimtaka hakimu “azingatie na kushikamana na ukweli” kwamba Bw Wa Iria amepelekwa kortini miaka 10 baadaye baada ya tarehe ya kuanza kwa kosa hilo analodaiwa kutenda.
Alisema kutokana na msukumo wa umoja wa vyama vya kisiasa, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye pia ni wakili, Bw Eugene Wamalwa, naibu kiongozi wa ODM ambaye pia ni gavana wa zamani wa Kakamega Wycliffe Oparanya, na Seneta wa Makueni Daniel Maanzo, walifika mahakamani kusimama na washtakiwa.
Waliitaka mahakama kuwaachilia kwa dhamana. Upande wa mashtaka haukupinga kuachiliwa kwao kwa dhamana.