Wa Iria: Hatutakusahau Matiba
Na GAVANA MWANGI WA IRIA
HABARI kuhusu kifo cha Shujaa wetu Mheshimiwa Kenneth Stanley Njindo Matiba ilinipata kwa mshangao mkubwa.
Kwa niaba ya wakazi wa Kaunti ya Murang’a, namwomboleza huku nikisherehekea maisha yake. Hamna shaka kuwa Mheshimiwa Matiba alikuwa kiongozi aliyeheshima kote nchini.
Alikuwa kilelezo cha kiongozi bora. Alikuwa mwanamapinduzi. Alikuwa mkongwe katika siasa za taifa hili. Alikuwa kiongozi jasiri na mwanamapinduzi. Historia yake ni hazina kubwa ambayo hatuwezi kuimaliza.
Lakini tunashukuru kwa miaka aliyoishi. Matendo yake na kauli mbiu zake za “Kuga na Gwika” (Kusema na Kutenda) na “Let The People Decide” (Watu wapewe Nafasi ya Kujiamulia) daima hazitasahaulika.
Hatasahaulika kwa sababu mchango wake katika vita vya ukombozi wa pili ni muhimu na hauwezi kumithilishwa.
Alikuwa na ndoto. Alipiga hatua na kufanikisha ndoto hiyo. Alilipia kwa kupoteza mali yake, na muhimu zaidi kuathirika kiafya.Na licha ya kupitia masaibu hayo yote, hakupoteza msukumo wake wa kupigania demokrasia na mageuzi ya kikatiba.
Mapambano, mchango na kujitolea kwake kwa harakati za kuboresha maisha nchini hauwezi kupuuzwa. Kwani daima yatakumbukwa katika historia ya taifa letu.
Tunaweza tu kumlipa kwa kuheshimu na kuendeleza mambo ambayo alithamini na kupigania.
Alikuwa wa kwanza kama mchapa kazi. Aliorodheshwa miongoni mwa wale waliopata ufanisi mkubwa kazini. Alikuwa katika tabaka la waliopata alama ya A+. Tabaka la wachache miongoni mwa wananchi ambao walijitolea kwa ajili kutetea masilahi ya umma. Ndiyo, alikuwa kiongozi wa aina yake.
Huku tukifurajia matunda ya mawanda mapana ya demokrasia yetu, kamwe hatutasahau mchango wake. Hajatuwacha. Kumbukumbu yake itadumu milele.
Alikuwa kilelezo bora aliyewakilisha hulka na mioyo ya watu wa Murang’a. Alionyesha moyo wa nidhamu, maadili kazini, kuwatenda watu wema, bidii, uwezo katika ujasirimali, umoja, usawa na uhuru.
Hii ndio maana tumemheshimu kwa kuanzisha hospitali kubwa ya macho na meno katika mji wa Kenol, Murang’a na kuipa jina lake. Hii ndio Hospitali kubwa ya aina yake katika eneo la Kati mwa Kenya.
Hospitali hii hutoa huduma bora katika eneo hili, alivyofanya marehemu Matiba.
Mungu aiweke Roho yake pema penye amani milele.