Habari Mseto

Waajiri waonywa dhidi ya kufuta wafanyakazi

March 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na VICTOR RABALLA

WAAJIRI wanaotumia vibaya hali iliyopo kuwafuta kazi wafanyakazi wao wameonywa vikali.

Huku biashara zikijaribu kupunguza gharama za malipo ya mishahara kutokana na athari ya mlipuko wa virusi vya corona, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu-K), Bw Francis Atwoli amesema kanuni mwafaka za leba zinapaswa kufuatwa.

Mkuu huyo wa Cotu aliyezungumza jijini Kisumu alihimiza mashirika ambayo yameathiriwa kuhusisha wadau katika jamii ili kudumisha mahusiano ya kudumu na mazingira bora ya kufanya kazi.

“Huku tukichukua hatua kadhaa za kujilinda leo, tunapaswa kujiandaa kutekeleza shughuli wakati virusi hivyo vitakapodhibitiwa hatimaye,” alisema Atwoli.

Aidha, alionya serikali dhidi ya kutekeleza hatua ya kufunga shughuli zote nchini ili kuzuia kusambaa kwa Covid-19.

Alisema kwamba hatua hiyo huenda ikalemaza uchumi hasa wakati huu ambapo taifa linakabiliana na nyakati ngumu kifedha.

“Hakuna mwanasiasa au gavana anayepaswa kuzungumza kuhusu kufunga uchumi wa taifa changa na dhaifu kama hili la Kenya. Hatua hiyo inaweza kuathiri vibaya wamiliki wa biashara ndogondogo na za wastan wanaotegemea wachuuzi, vioski na wafanyakazi katika sekta ya juakali,” alisema.

Akizungumza katika Chuo cha Mafunzo ya Leba cha Tom Mboya, afisa huyo wa vyama vya wafanyakazi aliwalaumu baadhi ya Wakenya wanaoeneza uvumi na kujaribu kuibua hofu na taharuki isiyofaa.

Huku akitoa wito kwa Wakenya kuchukua hatua za kutosha kuzuia maradhi hayo hatari ya Covid-19, alisisitiza kwamba virusi hivyo vinaweza kudhibitiwa kirahisi.

“Tunapaswa kuwahimiza watu kufanya kazi yao, kuendelea na biashara zao na kujihadhari. Hata inapothibitishwa kwamba mtu ana ugonjwa huo, anapaswa kutafuta matibabu,” alisema.

Katika hafla hivyo, Muungano wa Waajiri wa Kilimo na Wafanyakazi wa Mashambani (KPAWU) ulitia saini mkataba wa maafikiano utakaohakikisha kwamba zaidi ya wafanyakazi 50,000 katika sekta ya kilimo hawaachishwi kazi katika kipindi hiki kigumu kiuchumi.

Kulingana na mkataba huo, wafanyakazi hao watapewa siku walizobakisha za likizo ya mwaka mara moja.

Kwa waajiriwa ambao hawajabakisha au hawana siku za likizo ambazo hazijasazwa, mashirika yatawapa likizo yao ya kila mwaka kabla ya wakati wake kuwadia.

Mkurugenzi wa muungano huo Wesley Siele pia aliashiria kwamba mchakato wa haki na urazini utatumiwa.