Habari Mseto

Wabakaji wapewe adhabu kali – mbunge

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

KESI za ubakaji zimezidi sana hasa eneo la Gatundu Kaskazini na serikali yastahili kuingilia kati, amesema mbunge.

Mbunge wa Thika, Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema kwa siku za hivi karibuni matukio ya aina hiyo yamezidi vijijini.

Alitaja eneo la King’oo na Gakoe ambako kesi za ubakaji ziliripotiwa chini ya muda wa wiki mbili zilizopita.

“Watu wengi wanaohusika na ubakaji huo wanajulikana na wakazi lakini wanaogopa kuwashtaki. Wengine pia ni jamaa zao wa karibu,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo mnamo Jumamosi katika mazishi ya mmoja wa walimu wa shule moja ya msingi eneo hilo.

Alisema wabakaji wanastahili kupewa adhabu kali ili wapate funzo kamili.

Aliwashauri maafisa wanaotwikwa jukumu la kuchunguza maswala ya ubakaji kutendea waathiriwa haki kwa kutoa ripoti kamili.

Waliobakwa pia walishauriwa wawe mstari wa mbele kuripoti matukio hayo.

Alisema wanawake katika eneo hilo wanaogopa hata kwenda kulima mashamba yao huku wakihofia wanaweza wakashambuliwa na wabakaji hao.

“Ni vyema serikali kuangazia jambo hilo kwa uzito kwa sababu ni kero kubwa kwa wanawake wa eneo hili,” alisema Bw Wainaina.

Alitoa mwito kwa wanawake waliobakwa kujitokeza na kuripoti jambo hilo ili wahusika wa unyama huo wakabiliwe vilivyo na sheria.

“Machifu pia wana jukumu la kushirikiana na wananchi mashinani ili kuwanasa wabakaji,” alisema Bw Wainaina.