Habari MsetoSiasa

Wabunge wa Jubilee wanaohujumu kazi ya Rais wakejeliwa

August 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Wabunge wa zamani kutoka Kaunti za Meru na Tharaka Nithi Jumanne walipuzilia mbali viongozi wanaopinga hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kumaliza ufisadi nchini.

Walimtaka Rais Kenyatta kuwafuta kazi wote wanaohujumu juhudi zake za kurejesha taifa linapofaa kuwa, kwa kumaliza ufisadi na hali ya kutojali.

Chini ya mwavuli, ‘Meru Handshake Forum’ wabunge hao walisema ilikuwa vibaya kwamba baadhi ya viongozi wa Jubilee wanahujumu juhudi za rais kupigana na ufisadi na hali ya kutojali.

“Tunaunga mkono mkataba kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga na madaraja ya umoja,” alisema mwakilishi wa kundi hilo Dkt Kilemi Mwiria, muda mfupi baada ya kukutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga afisini mwake, Capitol Hill.

Walimtaka Rais Kenyatta kutotishiwa na watu waliodai ni wafisadi na kumtaka kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya wote wanaohusika katika ufisadi.

Walisema sababu ya baadhi ya wabunge kumpinga rais katika vita dhidi ya ufisadi na hatua alizochukua kutwaa maeneo ya mito inatokana na kuwa kiongozi huyo analenga kurekebisha mabaya yaliyofanywa awali.

Waliwakosoa baadhi ya wabunge wa Jubilee kwa kusema kazi yao imekuwa ni kumtusi Raila Odinga kila Jumapili wanapoenda kanisani kwa harambee, “ambazo zimekuwa ibada yao.”

Kundi hilo la wabunge wa zamani 12 na wawaniaji walioshindwa kutoka Meru, pamoja na wafanyibiashara kutoka eneo hilo liliahidi kumshika mkono Bw Odinga iwapo ataamua kugombea urais 2022.

Waliunga serikali mkono kwa hatua ya kutwaa Msitu wa Maasai Mau na ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kando au juu ya mito.