• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Wabunge wahimizwa kuinua maisha ya vijana wenzao

Wabunge wahimizwa kuinua maisha ya vijana wenzao

Na SAMUEL BAYA

SPIKA wa Seneti, Bw Kenneth Lusaka amewataka wabunge vijana kupeleka miswada inayolenga kuboresha maisha ya vijana nchini.

Akiongea alipofungua rasmi warsha ya siku mbili ya wabunge hao katika hoteli ya Whitesands Sarova, Kaunti ya Mombasa, Bw Lusaka alisema kuwa kuna mengi ambayo wabunge hao wanafaa kutekeleza kulinda masilahi ya vijana wenzao mashinani.

Vile vile aliwataka wajitahidi kupigana na ufisadi ili taifa hili lijikomboe kutoka kwa tatizo hilo linaloathiri uchumi na maisha ya wananchi.

“Ufisadi huanzia utotoni pale ambapo wewe kama mzazi unampa mtoto wako peremende ndipo aende sokoni unapomtuma. Kisha wizi utaanzia kwa kuiba kijiko kimoja cha sukari na hata baadaye uibe kiwanda kizima cha kutengeneza sukari. Haya ndiyo mambo ambayo lazima tuayaanglaie kama wabunge vijana,” akasema Bw Lusaka.

Spika huyo ambaye alieleza safari yake tangu akiwa mkuu wa tarafa hadi kuwa Gavana na sasa spika, alisema kuwa wabunge vijana lazima wasaidie wenzao mashinani kupambana na maisha bila kusita.

“Niko na furaha kwamba nyinyi kama vijana wabunge mumeamua kushirikiana kutoka mabunge yote mawili (Bunge la Taifa na Seneti) kuja pamoja na kusukuma maendeleo. Nina matumaini makubwa kwamba mwelekeo huu utaendelea hata katika bunge lijalo,” akasema Bw Lusaka.

Naye Seneta wa Nairobi Bw Johnson Sakaja aliwaambia wabnuge wenzake kwamba baada ya mafunzo wawe tayari kwenda mashinani kuwatia shime vijana wenzaao.

“Warsha hii ni ya mafunzo na baada ya mafunzo haya, hatua itakayofuata ni yenu kwenda kwenda mbele na kuwatia shime vijana wenzenu katika maeneobunge na kaunti mnazowakilisha,” akasema Bw Sakaja.

Aidha Seneta huyo alilaumu ufisadi kuwa chanzo cha masaibu mengi ambayo vijana wanapitia na akasema kuna haja ya kuhakikisha kwamba masuala muhimu yanayogusa maisha ya vijana yanashughulikiwa.

“Vijana wetu kule nje wanapitia masaibu mengi, baadhi yao yakiwatisha tamaa. Sasa kilochomo ni kuhakikisha kwamba tunapata viongozi ambao watahakikisha kwamba ndoto za vijana hawa zinatimia,” akasema Bw Sakaja.

Aliongeza kwamba ufisadi umewafanya vijana wengi kukosa ajira katika idara ya serikali mbali na kuifanya sekta ya kibinfasi pia kulemewa na matatizo.

“Tunachosema ni kuwa lazima sasa tupigane na ufisadi kwa kila njia pasipo kuweka masuala ya ukabila au mirengo ya vyama,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaelekeza macho Amerika kusaka wafadhili

Kesi ya mauaji ya Ivy yavutia mashahidi zaidi ya 10

adminleo